News

KONGAMANO LA AFYA NA UZINDUZI WA MPANGO MKAKATI WA MIAKA MITANO WA TAASISI YA BENJAMIN WILLIAM MKAPA (2019-2024)

BENJAMIN WILLIAM MKAPA FOUNDATION

YAH: KONGAMANO LA AFYA NA UZINDUZI WA MPANGO MKAKATI WA MIAKA MITANO WA TAASISI YA BENJAMIN WILLIAM MKAPA (2019-2024)

 

Katika kuchangia utekelezaji wa vipaumbele vya  Serikali ya awamu ya tano vya uboreshaji wa huduma kwa wananchi ,Taasisi ya Benjamin William Mkapa katika siku ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano ijayo ( 2019-2024)  iliwakutanisha wadau  kujadiliana masuala mbalimbali ya afya, ili kuweza kufikia malengo ya Maendeleo endelevu ( Sustainable Development Goals) na Afya kwa Wote ( Universal Health Coverage). Mijadala hiyo iliyoendeshwa na Taasisi kupitia watalaam mbalimbali wa sekta ya afya, imeshirikisha Serikali za Tanzania, Wadau wa Maendeleo, Mashirika yasiyo ya kiserikali yakiwemo ya dini na sekta binafsi.

 

Mijadala hiyo ilitanguliwa na mwongozo kutoka kwa mgeni mzungumzaji (Guest Speaker),  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile kwa kutoa mwelekeo wa dunia, Afrika na Tanzania katika kimarisha ustawi wa wananchi ili kufikia malengo hayo ya kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mojawapo iliyoridhia.

 

Dkt Ndungulile alibainisha kuwa Tanzania ipo katika hatua nzuri kufikia malengo hayo ya kimataifa na kitaifa kama ilivyodhihirishwa na tathmini ya utekelezaji wa mikakati iliyowekwa katika Mpango Mkakati wa Nne wa miaka mitano wa Sekta ya Afya. Dkt. Ndugulile alisema pia Serikali kwa sasa inalenga kuimarisha zaidi huduma za kinga za magonjwa ya kuambikiza sambamba na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo ni tatizo linalokuja kwa kasi kubwa na inagharimu Serikali na familia fedha nyingi katika kupata matibabu husika.

Aidha Dkt Ndugulile alisisitiza wadau kuendelea kufanya kazi na Serikali ili kuhakikisha malengo yaliyofikiwa yanakuwa endelevu na yale yaliyosalia yanafikiwa kwa kiwango madhubuti wakati Serikali itakapoanza kutekeleza mkakati ujao wa tano wa Sekta ya afya.

 

Pamoja na hilo Mhe. Naibu Waziri alitoa pongezi na kuitaka Taasisi ya Mkapa Foundation na wadau wengine kuendelea na progamu za kuimarisha upatikanaji wa watumishi wa afya wenye sifa ikiwa ni mkakati wa kuisaidia Serikali katika kupunguza uhaba wa watumishi wa afya uliopo nchini, ambayo ni moja ya nguzo kuu ya kufikia malengo ya Afya kwa Wote.

 

Nae Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Tanzania wa awamu ya tatu ambaye pia ni msarifu wa Taasisi ya Mkapa Foundation, Mhe. Benjamin William Mkapa alitoa shukrani zake za dhati kwa wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na Taasisi ya BMF ili kuweza kufikia malengo waliojipangia kama Taasisi. Hali kadhalika Mhe. Mkapa ameipongeza Serikali ya Awamu ya tano chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. John. Pombe Magufuli, kwa  kuimarisha mifumo ya afya ikiwemo upanuzi wa miundo mbinu ya vituo vya tiba zaidi ya 400 vinavyotoa huduma ya msingi maeneo mbalimbali nchini, kwa nia ya kufikisha huduma kwa wote.

 

Miongoni mwa shughuli nyingine iliyofanyika siku hiyo ni pamoja na uzinduzi rasmi wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa utakaotekelezwa kwa miaka mitano ( Julai 2019- Juni 2024) . Mpango huu umekuja na kauli mbiu isemayo kuelekea mifumo imara ya afya “Towards Stronger Health Systems” na umejikita katika kuhakikisha nchi inafikia malengo ya maendeleo ya kitaifa na ya kimataifa.

 

Dkt. Ellen Mkondya Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya BMF alisema, Mpango Mkakati huo umezingatia mabadiliko ya magonjwa na teknolojia, maendelo ya kiuchumi nchini na duniani, hivyo utagusa mahitaji na changamoto za utoaji afya ngazi zote, na hivyo kuendelea kuifanya Taasisi ya Mkapa kuwa chachu ya kutatua changamoto zilizopo kwa sasa na kuleta mbinu mbadala.

 

Aliongeza kwa kusema, ili kuendana na mahitaji ya kisekta ya sasa, Dira ya BMF itakuwa “Maisha yenye Afya njema na ustawi wa watu wote wa Tanzania na Afrika” (Healthy Lives and well-being in Tanzania and the rest of Africa)) na Dhima yake ni “Kuchangia katika kufikia matokeo bora ya kiafya, kwa kupitia ubunifu na suluhisho la mifumo husika”. (To contribute towards attainment of better health outcomes through innovative health and related system solutions) 

Aidha Taasisi italenga kufikia malengo makuu matatu ambayo ni:

  1. i) Uboreshhwaji mifumo ya kuongeza kasi ya kufikia malengo ya Kitaifa ya Afya Kwa Wote
  2. ii) Matumizi mathubuti ya taarifa kwa kubuni mikakati yenye matokeo

iii)        Kuongeza utendaji wa kitaasisi na uendelevu

 

Hali kadhalika BMF inatarajia kuendesha mikakati ya kuchangia nguvu za Serikali na wadau wengine katika kuimarisha mifumo ya afya ili kuwa endelevu na kuleta tija hususan, masuala ya upatikanaji wa watalaam wa afya katika ngazi ya vituo na kwenye jamii; kuhakikisha ongezeko la wananchi wenye bima ya afya;, kuimarisha uongozi na utawala bora wa ngazi za hospitali na vituo vya tiba, na kuimarisha upatikanaji na menejimenti ya rasilimali watu na fedha katika ngazi zote za vituo vya tiba.

Hali kadhalika uimarishaji wa huduma za kinga na tiba zitapewa kipaumbele na Taasisi ya BMF ikiwemo afya ya uzazi, magonjwa yasiyo ya kuambukizwa na magonjwa ya kuambukiza yakiwemo,  Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria

Pamoja na hilo Taasisi itajikita katika utafiti na matumizi ya taarifa ambazo zitasaidia katika kuhabarisha, kuchochea mabadiliko chanya na kuimarisha utengenezaji na utekelezaji wa mikakati ya kisekta pamoja na sera mbalimbali za Serikali.

 

Aidha Dr. Senkroo aliongeza kwa kusema kwamba Taasisi pia itajikita kujiimarisha zaidi mifumo, sera na miundo yake ya ndani ya Taasisi, ili kuwa na utendaji mahiri zaidi wenye ufanisi na weledi, na unaozingatia huduma kwa mteja, haki na ushirikiano.

 

Wakati wa mdahalo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dkt. Adeline Kimambo alisema kwamba ni dhahiri kuwa BMF ina uzoefu mkubwa katika utendaji wake na imeweza kuwanufaisha kwa njia moja au nyingine takribani watu milioni 11 kwa miaka 13 sasa tokea kuanzishwa kwake. Hivyo aliomba ushirikiano endelevu na wadau wote ili kuweza kufanikisha dira ya Taasisi na hivyo kuwatumikia vizuri zaidi wananchi.  Kufanikiwa kwa mpango huu kutatokana na ushirikishwaji na ushiriki wa Serikali, washirika wa maendeleo, wanataaluma, watafiti, sekta binafsi, mashirika ya dini, vyombo vya habari, jamii na wadau kwa ujumla wake.

 

 

Imetolewa na Menejimenti ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa

1 Oktoba 2019

 

 

Leave a Reply

Facebook

Twitter