'Afya kwa wote- Juhudi za Mzee Mkapa mwendelezo mpaka sasa'
Huenda ikakuchukua dakika 10 kuisoma makala hii, na kama ni hivyo wakati unamaliza kuisoma kuna watu Zaidi ya 68 duniani watakuwa wamepoteza maisha kwa sababu yakushindwa kulipia huduma bora za afya. Kinachosikitisha zaidi, vifo hivi vingi hutokea kwenye nchi masikini, ambapo idadi ya watu ambao hawawezi kuzifikia huduma za afya bado ni kubwa, na juhudi za kupunguza idadi hii zimekuwa za polepole sana.
Tanzania ni moja kati ya nchi 189 duniani zilizosaini makubaliano ya kufikia malengo ya maendeleo ya milenia (Sustainable Development Goal – SDG) kufikia mwaka 2030. Katika malengo haya 17, lengo namba 3.8 linasisitiza upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wote, bila kujali uwezo wa mtu kugharamia huduma hizo, kwa kifupi likisomeka Afya kwa Wote (universal health Coverage). Ukifatilia ripoti za umoja wa mataifa, sio nchi nyingi ambazo zitaweza kufikia lengo hili, na pengine Tanzania itakuwa ni moja ya nchi hizo.
Hapa Tanzania juhudi za kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma za afya zilianza tangu wakati wa Uhuru. Azimio la Arusha mwaka 1967 liliweka misingi ya ujamaa katika kujenga uchumi . Huu ulikuwa ni mwanzo wa mfululizo wa mabadiliko (reforms) katika sector ya afya yenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila mtu bila kujali hali ya kipato, dini, kabila au eneo analotoka. Hii iliendana na ujenzi wa miundombinu na kuongeza watumishi wa afya. Azimio la Arusha lilifuatiwa na uamuzi wa serikali kupiga marufuku huduma za afya zinazotolewa na watu /makampuni binafsi (private sector) na kuanzishwa kwa huduma za afya bila kulipia kwa ngazi zote za utoaji wa huduma za afya.
Mabadiliko mengine kwenye utoaji wa huduma za afya yalitokea mwanzoni mwa miaka ya tisini, ambapo kupanda kwa gharama za afya, kuongezeka kwa idadi ya watu na kuyumba kwa uchumi kulisababisha huduma za afya zinazotolewa kuwa duni, hivyo kulazimisha serikali kuanzisha utaratibu wa kuchangia huduma za afya, kabla ya kupata huduma. Ikumbukwe kuwa kupitia kodi, kila mtu tayari anachangia huduma za afya isipokuwa tofauti hapa ni kuwa unalazimika kulipa wakati umekwenda kwa matibabu kwenye kituo cha kutoa huduma za afya.Utaratibu wa kuchangia huduma ulianzishwa kwa awamu nne (4), kuanzia mwaka 1993 ulipoanza kwenye hospitali za rufaa hadi mwaka 1995 ulipoanza kutumika kwenye zahanati na vituo vya afya.
Uongozi wa awamu ya tatu, chini ya Rais Mh. Benjamin Mkapa unatambulika kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ambayo ilichangia kuleta mabadiliko mengi chanya kwenye uchumi wetu na huduma za Jamii. Ndicho kipindi ambacho mamlaka ya mapato (TRA) na mashirika mengine yaliyo ongeza tija katika utendaji wa serikali yalianzishwa. Pengine mabadiliko (reforms) makubwa na yaliyoacha alama kwenye sekta ya afya tangu Uhuru ni kuanzishwa kwa bima ya afya kwa umma (social health insurance), inayosimamiwa na shirika la NHIF wakati wa kipindi cha awamu ya tatu. Maandiko mbali mbali yanaelezea kuwepo kwa bima ya afya ya umma kama ndio njia rahisi na ya haraka ya kuweza kufikia afya kwa wote (UHC). Ukiacha nchi zilizoendelea ambako mfumo huu wa bima upo kwa miaka zaidi ya hamsini, na walishaweza kufikia afya kwa wote miaka mingi iliyopita, upande wa Afrika – kusini mwa Jangwa la sahara, nchi mbili ambazo zinafanya vizuri ni Rwanda na Ghana, zote zikinufaika na kuwepo bima ya afya ya umma iliyo imara.
Hata hivyo, sio jambo rahsi kuanzisha bima ya afya katika nchi na ndio maana licha ya kujulikana ni moja ya silaha muhimu ya kufkia afya kwa wote, nchi nyingi bado hawajaweza kuanzisha. Hapa kwetu pia kuanzishwa kwa NHIF kulikutana na mapingamizi kutoka kwa wadau wote muhimu. Wakati ambapo watumishi wa umma waligoma kukatwa fedha ili kujiunga NHIF, watoa huduma za afya nao walilalamikia malipo wanayopata kutoka kwa NHIF, hata kutishia kuacha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF. Hata wadau wa maendeleo pia mara kadhaa walipinga kuanzishwa kwa NHIF, kwa maelezo kuwa mfumo wa bima ya afya ya jamii hauwezi kufanya kazi kwenye nchi maskini. Kama sio Rais Benjamin Mkapa kusimama kidete, huku akiendelea kusimamia alichokiamini pengine leo tusingekuwa tunafurahia matunda ya NHIF. Nakumbuka kwenye sherehe za Mei mosi za mwaka 2002 Mheshimiwa Rais akiwa Mgeni rasmi, risala iliyosomwa na chama cha wafanyakazi ilipendekeza kusimamishwa kwa utaratibu wa watumishi kukatwa mishahara ili kulipia NHIF. Kwa ujasiri mkubwa, mheshimiwa Rais aliikingia kifua NHIF, na kusisitiza matatizo yanayotajwa yanatakiwa kufanyiwa kazi kuifanya bima ya afya ya umma imara, na sio kuufuta mfuko. Leo hii, ni mtumishi gani wa serikali utamwambia asikatwe NHIF na kisha ajilipie huduma za afya mwenyewe atafurahia hali hiyo? Na ni hospitali gani leo utawashauri wasitibu wagonjwa wa NHIF wakakubaliana na wewe? Ni maono ya mheshimiwa Mkapa yaliyotufikisha hatua hii ambayo inapelekea nchi mbalimbali kuja kujifunza uendeshaji wa bima ya umma Tanzania.
Pamoja na mafanilkio makubwa yaliyofikiwa na NHIF, labda suala la kujiuliza ni kuwa kwanini mpaka sasa Tanzania tuko nyuma sana kwenye juhudi za kufikia afya kwa wote? Ukiangalia mpaka sasa watu wenye bima za afya ni asilimia kumi na mbili (12) tu! Kati ya hao, asilimia 8 wako NHIF, asilimia 3 wana kadi za iCHF na asilimia moja wana bima ya afya za kampuni binafsi.
Nadhani changamoto ilikuwa hatukuweza kuendelea pale tulipoishia mwaka 2005. Tatizo kubwa limekuwa ni kukosa utashi wa kisiasa kwenye kufikia afya kwa wote. Pamoja na kuwa kila uchaguzi ukifika vyama vyote vikubwa vimekuwa na agenda ya afya kwa wote kwenye ilani zao, utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua. Ikumbukwe kuwa, NHIF ilianzishwa kisheria kwa ajili ya watumishi wa umma. Baada ya kuimarika kwa NHIF, ilitakiwa kuwe na muendelezo wa kuanzisha sheria ya ulazima wa bima ya afya kwa watu wote. Sheria ya ulazima wa bima ya afya imekuwa ikipigwa kalenda kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Kwa bahati nzuri, karibuni tumeona mabadiliko kwenye hili, na kikao cha juu cha chama tawala kimelipokea na kulibariki suala la afya kwa wote. Pengine sasa jambo hili lililosubiriwa kwa Zaidi ya miaka kumi, litafika mwisho na tutakuwa na sheria itakayolazimisha bima kwa watu wote.
Hata hivyo, pengine kosa kubwa ambalo tutafanya ni kudhani kuwa kupitishwa kwa sheria ya ulazima wa bima tu peke yake ndio itakuwa suluhisho la upatikanaji wa afya kwa wote. Ili kufanikiwa, Sheria ya ulazima wa bima ya afya lazima iandaliwe mazingira yatakayovutia watu waweze kujiunga na bima ya afya. Ukihesabu nchi za kusini mwa jangwa la Sahara zenye sheria kama hii hazipungui tano, kati ya hizo iliyofikia afya kwa wote ni moja tu, Rwanda na wengine wanaokaribia ni Ghana. Ni kipi kinatofautisha waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa?
Kwanza ni lazima serkali iweke utaratibu madhubuti wa kuwalipia ambao hawana uwezo. Licha ya uwepo wa sheria, kuna idadi kuwa ya watu ambao kutokana na umaskini hawataweza kujilipia. Kundi hili kwenye nchi zilizofanikiwa huwa wanalipiwa na serikali (premium subsidy). Kwa Tanzania bara, kundi hili linakadiriwa kufikia asilimia 18 ya watanzania wote. Suala la kwanza ni kuwatambua, ili kuhakikisha serikali inalipia walengwa. Baada ya kuwatambua ni muhimu serkali iwe na chanzo endelevu na uhakika cha mapato kuwezesha kuwalipia ada ya bima kundi hili. Hatutafanikiwa kwa kutumia hela zinazotengwa kutokana na utashi wa mtu, au watu wachache. Ni muhimu sheria ya kodi ielekeze kuwe na sehemu ya mapato ya kodi ambayo itatengwa kama chanzo cha mapato kulipia kundi hili. Mfano, Ghana wanatumia asilimia 2.5 ya VAT kulipia kundi kama hili wakati Rwanda wao wamechagua kodi/tozo zaidi ya tano zinazochangia mfuko wa kulipia kundi hili. Kwa maana hiyo, ili kufanikiwa sheria ya ulazima wa bima lazima iendane na mabadiliko kwenye sheria ya kodi.
Jambo lingine la msingi ni umakini kwenye kuchagua kitita cha mafao (benefit package), kinachotumika katika sheria ya afya kwa wote. Ikumbukwe kuwa kiasi cha gharama watakayolipa watu kujiunga na bima hii inachangiwa kiasi kikubwa na kitita cha mafao. Takwimu zinaonyesha Zaidi ya 80% ya watu wanaotumia huduma za afya huhitaji kupata huduma za afya ya msingi pekee. Wachache huhitaji huduma za rufaa na wachache zaidi huhitaji huduma za kibingwa. Chukulia mfano wakulima 50 walilazimishwa kupanda basi la kwenda Morogoro na pamoja na wafanyabiashara wakubwa 4. Wakulimam walikuwa wanashuka KIbaha, lakini walilipa nauli sawa na wale wafanyabashara 4 wanaoenda mpaka Morogoro. Maana yake watu 50 wenye kipato kidogo wameumia kwa ajili ya kuwasaidia wanne ambao pengine hawakuhitaji huo msaada kutokana na kipato chao. Inaeleweka kuwa msingi wa bima ni kuchangiana, lakini haina maana kama kuwepo kwa baadhi ya huduma kutasababisha gharama iwe kubwa hivyo asilimia kubwa ya watu washindwe kujilipia. Lengo tunataka tuwe na asilimia 80 ya watu wajiunge na bima, hivyo bei lazima iwe rafiki. Mfano mzuri ni Rwanda, ambao bima yao inayotoa huduma za afya ya msingi (Mutuelle) inagharama ndogo za kujiunga kiasi cha kuwezesha zaidi ya asilimia 80 kujiunga. Pia, ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi, serikali lazima iendelee kuchangia (kupitia mfuko wa bima) baadhi ya huduma ambazo au zina gharama kubwa sana (mfano magonjwa sugu) au huduma zinazoweza kutabirika (mfano; ujauzito).
Kuchagua kitita cha mafao, inaendana na uchaguzi mzuri wa namna ambavyo msimamizi wa bima atawalipa watoa huduma. Iko mifumo tofauti ya kulipa watoa huduma, na mara nyingi watoa huduma hupendelea ile mifumo ambayo huwapa wao faida Zaidi. Ni jukumu la mtoa bima kuchagua mfumo sahihi utakaowalinda wanachama wake na kulinda uhimilivu wa mfuko. Zipo njia zinazofahamika kuwa zina manufaa zikitumika kwenye afya ya msingi, mfano ni njia ya capitation. Hata hivyo sio watoa huduma wengi wanazipenda sababu inawalazimisha kuongeza umakini kwenye huduma na gharama wanazotumia. Unahitajika uthubutu kuweza kuanzisha na kusimamia njia hizi ambazo ukizianzisha lazima utakutana na mapingamizi, lakini muhimu kwa uhimilivu wa mfuko, hasa kama unalengo la kuwafikia Zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 60.
Pia kuna suala la kuwa na huduma rafiki kwa watu kujiunga. kuwalazimisha watu kulipia gharama ya kujiunga bima ya miezi 12 huku ikifahamika kuwa vipato vya watu wengi ni vya kila mwezi, wiki au siku, ni tatizo linalohitaji ufumbuzi.lazima mfumo wa kulipia uwe rafiki kwenye kulipia, hasa ikizingatiwa mifumo ya technolojia na simu imerahisisha sana udhibiti kwenye huduma.
Upande wa pili kwenye afya kwa wote ni kwenye utoaji wa huduma za afya. Pongezi nyingi kwa serikali ya awamu ya tano nah ii ya sita kwa juhudi kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu. Pamoja na hayo, inahitajika juhudi kama hiyo kwenye uboreshaji wa huduma hasa upande wa watumishi, vitendea kazi na upatikanaji wa dawa. Upande wa dawa na vitendea kazi ni eneo la msingi Zaidi na linalohtaji uharaka. Pengine kuna haja ya kuangalia mfumo wetu mzima wa usambazaji wa dawa kwenda kwenye vituo, kuondokana na huu wa sasa ambao serikali hupeleka hela bohari ya madawa na kuwataka bohari wasambaze dawa vituoni, tutumie mfumo ambao hela ziende kwenye vtuo vya kutolea huduma kupitia bima na kuwataka watoa huduma wenyewe waagize na kulipia dawa toka bohari ya madawa. Unakumbuka mara ya kwanza ulipoanza kujitegemea ulipokuwa unatumia vitu unavyonunua kwa umakini kulinganisha na siku ulizokuwa nyumbani kwa wazazi? Pengine hili litatokea kama watoa huduma iwapo watatakiwa kulipa wenyewe dawa wanazonunua. Lazima tukubali kwa sasa kuna upotevu mkubwa wa dawa, pamoja na wingi wa dawa zinazoharibika bila kutumiwa.
Kuna mengi ya kuandika, lakini pengine sitatendea haki Makala hii kama sitaongelea umuhimu wa matumizi ya takwimu. Matumizi ya takwimu yanaweza kutusaidia kwenye maeneo mengi kufikia afya kwa wote, mojawapo ni kuwatambua wasio na uwezo wa kujiunga na bima. Kwa kutumia taarifa za matumizi ya simu (muda wa maongezi, hela unazopokea/kutuma kwenye simu, matumizi ya internet nk) watafiti wanaweza wakawatambua kipato cha mtu na hivyo kujua uwezo wake wa kujilipia na bima. Lakini pia takwimu zinaweza kusaidia kuwafikia walengwa (targeted marketing) kwa ujumbe sahihi utakaowafikia wakati sahihi, ili waweze kujiunga na bima huku pia zikiwezesha malipo kufanyka tokea sebuleni kwa wateja. Halafu kuna matumizi ya takwimu zinazoletwa na watoa huduma ili walipwe madai. Eneo la matumizi mabaya ya dawa, matibabu yasiyo ya lazima na hata namna bora ya kudhibiti gharama za matibabu zinaweza kuboreshwa kutumia takwimu.
Afya kwa wote inawezekana, ni suala ambalo lipo ndani ya uwezo wetu. Kama ambavyo Rais Mkapa alithubutu na kusimamia uanzishwaji wa mfumo wa afya kwa Jamii (social health insurance), kinachotakiwa ni aina kama hiyo ya uthubutu ili kutuvusha eneo lililobakia kufikia afya kwa wote sababu misingi tayari ilishawekwa tangu mwaka 2001 wakati tulipoanzisha NHIF, tuanzie pale tulipoishia mwaka 2005.