HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI;
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KATIKA HAFLA YA KUFUNGA KONGAMANO LA PILI LA KUMUENZI HAYATI MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, RAIS WA AWAMU YA TATU YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA – GOLDEN TULIP AIRPORT HOTEL- ZANZIBAR.
TAREHE 14 JULAI, 2022,
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dr. Philip Mpango;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mzee Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji
Mheshimiwa Othman Masoud Othman; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa;
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Zuberi Ali Maulid; Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Amani Abeid Karume; Rais Mstaafu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dr. Mohamed Gharib Bilal;
Makamu wa Rais Mstaafu wa Jahmuri ya Muungano wa
Tanzania
Mheshimiwa Mama Anna Mkapa; Mjane wa Mheshimiwa Rais Mstaafu Marehemu Benjamin William Mkapa,
Waheshimiwa Wake wa Viongozi wastaafu;
na waliopo Madarakani,
Waheshimiwa Mawaziri na Viongozi Wakuu wa Serikali; Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na Wajumbe wa Bodi ya
Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF);
Waheshimiwa Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya ya Wanadiplomasia;
Dkt. Ellen Mkondya Senkoro; Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi
ya Benjamin William Mkapa (BMF),
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana!
Assalam Aleikum
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya shughuli hii ya kulifunga Kongamano hili la pili la kumuenzi Hayati Benjamin William Mkapa ikiwa ni sehemu ya Kumbukizi ya pili ya Hayati Mzee Benjamin William Mkapa.
Mtakumbuka, mwaka jana wakati wa kumbukizi ya kwanza, nilielezea azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa kumbukizi ya pili ya Hayati Mzee Benjamin William Mkapa. Nina furaha kuona kwamba, tumeweza kutekeleza ahadi yetu hiyo hapa Zanzibar kwa ufanisi mkubwa kama tulivyoshuhudia jana na leo.
Kwa namna ya pekee, nami nikiwa Msarifu mpya wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, nachukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kuhudhuria Kumbukizi hii. Tunafahamu namna ratiba yako ilivyosheheni shughuli nyingi za Kitaifa. Hata hivyo, kwa heshima na mapenzi makubwa uliyonayo kwa Mzee wetu Hayati Benjamin William Mkapa pamoja na Zanzibar, umeona umuhimu wa kuhudhuria wewe mwenyewe kwenye kumbukizi hii. Tunakushukuru sana.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Kwa upande mwengine, natoa shukrani kwa Wazee wetu Marais Wastaafu, Mheshimiwa Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji na Viongozi wastaafu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuja kuhudhuria katika shughuli hii. Ushiriki wenu umezidi kuipendezesha na kuipa uzito shughuli hii.
Nyinyi mmefanya kazi na hayati Mzee Mkapa kwa karibu katika shughuli mbali mbali za Kikanda na Kimatafa, jambo ambalo liliwezesha kujenga urafiki wa karibu baina yenu, na bila shaka, mliweza kubadilishana nae mawazo katika masuala muhimu ya maendeleo na kisiasa. Tunakushukuruni sana kwa uwepo wenu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Nachukua nafasi hii, vile vile kutoa shukrani kwa Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa pamoja nasi. Shukrani zangu ziende kwa viongozi wote wa Chama na Serikali pamoja na Wanafamilia ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ikiongozwa na Mama Anna Mkapa. Kadhalika, natoa shukrani kwa washirika wetu wa maendeleo kutoka jumuiya na taasisi mbali mbali, Ofisi za kibalozi na mashirika ya Kimataifa. Aidha, shukrani maalum nazitoa kwa Bodi na Menejimenti ya Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana vyema na watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja mkaweza kufanikisha maandalizi ya shughuli hii, na hatimae ikaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa kama tunavyoshuhudia hapa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Kumbukizi hii ya pili ina nafasi adhimu kwangu. Kwanza, ni mara ya kwanza ninakuwa mwenyeji wa kumbukizi hii. Pili, ni mara ya kwanza pia kuhudhuria Kumbukizi hii nikiwa Msarifu (Settlor) wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa. Leo napenda nihadithie kwamba, wakati nilipofuatwa kuombwa kuwa Msarifu nilipata kigugumizi kukubali. Kigugumizi changu kilitokana na mashaka kuwa viatu ninavyovivaa ni vikubwa ikizingatiwa kwamba Msarifu wa kwanza alikuwa ni yeye mwenyewe Hayati Mzee Mkapa.
Sikuwa na njia wala uthubutu wa kukataa dhima ya jukumu la kuwa msarifu. Nilipata nguvu zaidi ya kukubali kuongoza taasisi hii nikitambua kuwa matunda ya kazi zinazofanywa na taasisi hii yanalenga kuimarisha ustawi wa Tanzania na kazi njema lazima iendelezwe. Kwa hivyo, kazi njema iliyoanzwa inaendelea ikiwa pia ni njia bora na sahihi ya kumuenzi na kumkumbuka Marehemu. Kwa kutambua dhima na ukubwa wa jukumu nililorithi, nimejizatiti kwa kadri ya uwezo wangu kuongoza taasisi hii na kuhakikisha kwamba dira na dhamira ya kuanzishwa kwake inafikiwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele cha kuimarisha ushirikiano na Sekta binafsi pamoja na Asasi za Kiraia. Vile vile, Suala la ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi limehimizwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050, Ilani ya CCM 2020 /2025 pamoja na mipango mengine ya maendeleo ya Kitaifa. Ninaendelea kufarijika kwa namna ambavyo sekta binafsi zikiwemo asasi za kiraia inavyoendelea kushirikikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo. Natoa shukrani maalum kwa viongozi pamoja na watendaji wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali zetu zote mbili katika kuimarisha huduma mbali mbali, hasa katika sekta ya afya. Kwa upande wa Zanzibar, Taasisi hii inafanyakazi kwa karibu na Wizara ya Afya katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma, utoaji wa mafunzo na hivi sasa katika kutekeleza mipango itakayotuwezesha kuanzisha Bima ya Afya hapa Zanzibar. Ni vyema asasi nyengine za kiraia zikaiga mfano huu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Ushirikiano mzuri ulokuwepo baina ya Serikali na sekta binafsi umesaidia sana katika juhudi zetu za kupambana na maradhi ya UVIKO- 19. Taasisi mbali mbali zinaendelea kushirikiana na Serikali katika upatikanaji vipimo, vifaa tiba, utoaji wa chanjo, elimu ya kinga, pamoja na ukusanyaji wa takwimu katika maeneo mengine mengi. Mafanikio haya yamezidisha imani ya wananchi juu ya umuhimu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi siyo tu katika uwekezaji, bali pia katika utoaji wa huduma za jamii.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Wakati tunamkumbuka Marehemu Mzee Mkapa, nachukua nafasi hii kugusia kidogo kuhusu falsafa na wosia aliotuachia kuhusu ujasiri na changamoto za kufanya mageuzi.
Katika kitabu chake, ‘My Life, My Purpose – A Tanzanian President Remembers’ akizungumzia ugumu aliokutana nao katika zoezi la kufanya mageuzi ya ubinafsishaji, Hayati Rais Mkapa ameandika (nanukuu),
“Kuwa kiongozi kunahitaji kuwa tayari kubadilika kuendana na mawazo mapya na kuwa na ujasiri wa kutekeleza yale yaliyo sahihi” (Uk. 139).
Ushupavu huu wa uongozi unajidhihirisha pia katika maneno ya Muasisi wetu wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar aliyesema, ninamnukuu
“Ni heri kugombana na mtu katika jambo tutakalokuja kupatana baadae”.
Kwa kawaida mageuzi, kama yalivyo Mapinduzi, huja na mafanikio na changamoto zake. Ni hulka ya binadamu pia kupenda kushikilia jambo alilozoea hata kama linamgharimu. Ndio maana wahenga wakasema, ‘mazoea yana tabu!’. Binadamu angelipenda yale mabadiliko tu ambayo hayaji na changamoto ama hayatibui mazoea yake. Bahati mbaya mawili haya hayatenganishwi.
Kwa kutambua hilo Serikali imedhamiria kushirikisha sekta binafsi katika nyanja zote za maendeleo sababu ni jambo sahihi kufanya hivyo. Tutaendelea kuwaelimisha wale wachache wenye mashaka, wakati tukiendelea kuzishirikisha sekta binafsi. Ni imani yetu, tutakuja kuelewana baadae. Wale ambao wanapata ugumu kutuelewa fikra na matendo yetu, watakuja kuyaelewa matokeo. Huo ndio ustahamilivu na ushupavu wa uongozi aliouzungumzia Hayati Mzee Benjamin William Mkapa na viongozi wetu wengine waliotutangulia. Nakuhakikishieni kuwa mimi na wenzangu tunao ustahimilivu na ushupavu huo.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa;
Nakiri kuwa nami nimefarijika sana na mjadala ulioanza hapa jana na kufunguliwa na Mheshimiwa Othman Masoud, Makamu wa Kwanza wa Rais. Nimeyapokea maazimio yaliyopitishwa na ninaahidi kwamba yale yote yanayoihusu Serikali tutayazingatia na yale yote yanayohusu Taasisi vile vile, nimeyachukua, na yote haya tutayafanyia kazi. Maazimio yaliyopitishwa yanatupa mwanga katika safari yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi na yanaimarisha misingi ya kuaminiana, kushirikiana, kutegemeana na kutumainiana kati za sekta za umma na sekta binafsi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Wageni Waalikwa;
Katika Kumbukizi ya kwanza mwaka jana tulianzisha Mfuko wa Wakfu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa (Endowment Fund). Natoa shukrani kwako Mheshimiwa Rais kuchangia katika mfuko huo. Umeonyesha njia. Nawashukuru wadau wengine wote waliotuchangia hadi leo.
Vile vile, jana usiku tulikuwa na hafla fupi ya kutunisha Mfuko huu wa Wakfu. Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba muitikio ulikuwa mzuri.
Tumefanikiwa kupata kiasi cha shilingi za kitanzania 1.2 b ikiwa ni pamoja na ahadi zilizotolewa. Sina shaka, kwamba wale wote walioahidi watatekeleza ahadi zao ndani ya kipindi kifupi kijacho. Kwa mara nyengine, natoa shukrani kwa wachangiaji wote.
Fedha zilizochangwa jana zitasaidia kuimarisha uwezo wa kifedha wa Taasisi, ambapo mfuko tayari una Shilingi za Kitanzania bilioni moja (1 billion). Kwa hivyo fedha hizo, pamoja na zile zinatolewa na wahisani mbali mbali zitakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango yetu ya kutanua wigo wa utoaji wa huduma, hasa katika maeneo ambayo hayakuwa yakipata ufadhili.
Ni matumaini yangu kwamba kwa kutambua kazi inayofanywa na taasisi hii katika kuimarisha ustawi wa wananchi, hamtochoka kushirikiana nasi katika kuutunisha mfuko wa Taasisi hadi pale utakapokuwa na uwezo wa kujiendesha wenyewe kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Wageni Waalikwa;
Kwa mara nyengine, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo ambao wanaendelea kushirikiana na taasisi hii tangu ilipoanzishwa. Kutokana na michango yenu, ambayo sasa imeshafikia takribani Bilioni 230 kwa miaka 16 iliyopita, tumeweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa program mbali mbali zilizowafikia wananchi katika Mikoa tofauti ya Tanzania bara na Zanzibar. Wadau hao ni pamoja na USAID, Global Fund, Irish Aid, UK-FCDO, Walter Reed, UNICEF, UNFPA, UNAIDS, AVAC, Abbott Fund, Serikali ya Norway, Ubalozi wa Japan na wengineo. Imani yetu ni kwamba mtaendelea kushirikiana nasi katika kupanga na kutekeleza mipango mbali mbali. Michango yenu ni mithili ya mbegu katika Taasisi yetu. Inaijenga Taasisi yetu kimifumo, kiutaalam na uwezo wa kujisimamia yenyewe siku zijazo.
Nikiwa Msarifu wa Taasisi hii, nawahakakishia kuwa kila senti mnayoitoa itatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa kama ambavyo tumekuwa tukitekeleza siku zote. Taasisi hii ni taasisi makini, inayowajibika na inasimamiwa na kuendeshwa kwa weledi. Muhimu zaidi, imejengwa juu ya mwamba imara wa fikra na falsafa za Hayati mpendwa wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa.
Tutamuomba Mwenyezi Mungu aiwezeshe Taasisi hii kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake na aijaze baraka na neema nchi yetu.