Hotuba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Raisi wa Tanzania.
Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kongamano la pili la kumuenzi Hayati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais wa Tatu wa Jamhuri Yya Muungano wa Tanzania, Tarehe 14 Julai, 2022, Golden Tulip Airport Hotel, Zanzibar
- Mheshimiwa Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania
- Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
- Mheshimiwa Othman Masoud, Makamu wa kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
- Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah, Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
- Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
- Waheshimiwa Marais Wastaafu (Wageni Wetu), Mzee Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji na Mzee Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini;
- Mheshimiwa Zuberi Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;
- Mheshimiwa Mama Anne Mkapa, Mjane wa Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa;
- Mheshimiwa Mariam Mwinyi, Mwenza wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar;
- Waheshimiwa Wake wa Viongozi wakiongozwa na Mama yetu Fatma Karume;
- Waheshimiwa Mawaziri na Viongozi Wakuu wa Serikali;
- Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF);
- Waheshimiwa Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya ya Wanadiplomasia;
- Dkt. Ellen Mkondya Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF);
- Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;
- Mabibi na Mabwana!
JAMHURI YA MUUNGANZO WA TANZANIAâĶ..!
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kuweza kukutana hapa leo kwenye shughuli yetu hii makhsusi ya kumuenzi Hayati Rais Benjamin William Mkapa. Ninayo furaha kubwa kujumuika nanyi kwa mara nyingine tena katika Kumbukizi ya Kuenzi Mchango wa Hayati Mpendwa wetu na Rais wetu wa Awamu ya Tatu. Mwaka jana tulijumuika pamoja kwenye Kumbukizi ya kwanza iliyofanyika pale ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Kwa kipekee nataka niwapongeze kwa kuwatambua na kuwashukuru waliochangia kufanikisha hafla hii ya leo ambao ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mashirika ya USAID, UNICEF, IPP Media, ZBC, Benki ya CRDB na wengineo.
Furaha yangu leo inachangiwa na mambo mawili makubwa. Kwanza, nimefurahishwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kutimiza ahadi yake aliyoitoa katika Kumbukizi ya mwaka jana kuwa, Kumbukizi ya Pili itafanyika hapa Zanzibar.
Pili, nimefurahishwa kwa Taasisi ya Benjamin William Mkapa kushirikiana na Serikali kuendeleza utamaduni huu wa kumuenzi Hayati mpendwa wetu Mzee Benjamin William Mkapa. Kufanyika kwa mara ya pili kwa Kumbukizi hii ni ushahidi kuwa tumedhamiria kuenzi mchango wake katika maendeleo aliyoyachangia katika Taifa letu, Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Rais na Msarifu (Settlor) wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa;
Nakupongeza wewe na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maandalizi na mapokezi mazuri ya wageni wetu waliokuja kujumuika nasi. Nitumie fursa hii kukupongeza vile vile kwa kukubali kuwa Msarifu (Settlor) wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa. Tunaamini viatu vilivyoachwa na Hayati Msarifu wetu Mzee Mkapa, vitakufaa sawa sawa, tukizingatia kuwa, wewe ndio pia ulikuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hii. Tunaimani unaijua Taasisi hii vyema, kwa kuwa wewe pia ni sehemu ya uasisi wake. Kwa hakika umemtendea haki Mzee Mkapa, na sina shaka huko aliko anafurahia na kujivunia kazi yako. Na sisi inatupa amani sana kuwa Taasisi hii iko kwenye mikono salama mno.
Mheshimiwa Rais,
Wageni Waalikwa;
Nimefarijika sana kuwaona Waheshimiwa Marais Wastaafu, Mzee wetu Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji; na Mzee Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini. Wazee wetu hawa walikuwa marafiki wa karibu wa Hayati Mzee Benjamin William Mkapa. Walipatana kifikra na walikuwa na urafiki uliojikita vyema katika udugu na umoja wa nchi zetu tatu. Misimamo yao aghlabu haikuwa ikitofautiana. Akiwepo mmoja kwenye Mkutano, hata kama mwingine hayupo, hakukuwa na shaka kuwa maslahi ya Ukanda wetu yatawasilishwa ipasavyo.
Uwepo wenu na sisi hapa leo, unadhihirisha hilo. Umejidhihirisha pia katika maneno yenu mazuri mliyoyatoa hapa ya kumuelezea rafiki yenu Mzee Mkapa. Mmetufuta machozi na kutupunguzia upweke. Tukiwaona tunafarijika na kuona kuwa tupo pamoja, na kwamba hatunaye Mzee Mkapa, lakini nyinyi wazee wetu mpo. Tukiwaona nyinyi, tunamuona yeye katikati yenu. Hamjatutupa! Tunamshukuru Hayati Mzee wetu kwa kutuachia marafiki na walezi wazuri. Karibuni sana!
Mheshimiwa Rais,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Nimevutiwa sana na kauli mbiu ya Kumbukizi ya mwaka huu inayosema, âUshupavu wa Uongozi katika Kuleta Mabadiliko kwa Manufaa ya Woteâ. Zaidi, ustahimilivu na ushupavu wa uongozi katika kuruhusu ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, katika kufanikisha lengo letu na lengo la tatu katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG 3) la kuhakikisha âHuduma ya Afya Bora kwa Woteâ (Universal Health Care) linafikiwa.
Binafsi, nilitamani sana kuwa sehemu ya mjadala uliofanyika jana uliofunguliwa na Mheshimiwa Othman Masoud, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, uliojikita kwenye kujadili nafasi ya sekta binafsi katika kuondosha changamoto za afya tulizonazo, na hatimae kuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea katika kulinda Afya za Watanzania. Matamanio yangu hayo yanatokana na imani kuwa ikiwa tunataka kwenda kwa kasi na kufikia lengo letu la 2030 la âAfya bora kwa Woteâ, basi hatuna budi kubadili mtazamo wetu kuwa tunaweza kulifanya hilo peke yetu. Lazima tufanyekazi pamoja na kwa mkakati bayana na wenzetu wa sekta binafsi.
Hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini thabiti wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutatua changamoto zinazotukabili. Alihubiri sana juu ya hili na pia aliutangulia wakati. Yumkini hatukumuelewa sana wakati ule. Sasa tunaendelea kumwelewa vyema. Muhimu zaidi, alikuwa na ushupavu wa uongozi katika mabadiliko hayo pamoja na kuwa yeye binafsi alikuwa muumini thabiti wa Ujamaa. Ila kwa wakati ule nchi ikiwa na Imani ya Ujamaa isiyoamini katika sekta binafsi.
Nakumbuka, katika Hotuba yake aliyoitoa katika Halmashauri Kuu ya CCM tarehe 25 Agosti, 2004 kule Dodoma, alizungumzia ushupavu wa uongozi unaohitajika katika karne ya 21. Katika Hotuba ile, pamoja na mambo mengine mengi, Mzee Mkapa alituasa kuwa (Nanukuu) âUongozi shupavu hauogopi kubadili mkakati iwapo ni lazima kufanya hivyoâ. Akaendelea kusisitiza kuwa, âTukishaamua sera tunahitaji ujasiri wa kutenda, si wa maneno. Ukiwepo ubishi uwe wa kasi na ubora wa utendaji, si wa sera tenaâ.
Mheshimiwa Rais,
Wageni Waalikwa;
Nimerejea maneno hayo ya Mzee wetu Hayati Benjamin William Mkapa kuonyesha maono yake katika ushupavu na ustahimilivu katika uongozi. Hakuogopa kutuambia ukweli kuwa dunia ya sasa ni dunia ya uchumi wa soko, na kwamba ubia na sekta binafsi ni jambo lisiloepukika. Sasa, tumelitambua hilo na kuliainisha katika Mikakati ya kitaifa ya maendeleo ya nchi yetu, ikiwemo pia katika Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya (Health Sector Strategic Plan – HSSP5 2021-2026). Tumetamka wazi kuwa tutashirikisha na kushirikiana na sekta binafsi zikiwemo pia Asasi za Kiraia, katika kufikia malengo yetu ya maendeleo ikiwa ni Pamoja na; kuwafikishia wananchi wote huduma bora ya afya, popote walipo, na kwa gharama wanazozimudu.
Tokea tuzindue Mkakati huu tarehe 17 Juni, 2021, sasa ni mwaka mmoja. Yafaa tujiulize: je, tumepiga hatua kiasi gani katika kushirikisha na kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kushiriki katika ubia na Serikali katika utoaji wa huduma bora za afya? Je, tunashirikiana na kushirikisha Sekta Binafsi katika tija za kimkakati za maendeleo ya kuichumi yenye kuongozwa na vielelezo, na sio hoja tu zisizotusogeza mbele? Vipi kuhusu matamko ya viongozi wetu mbalimbali juu ya ukuu wa Serikali katika kutekeleza mkakati huu au utoaji wa huduma za afya? Je, maneno, matendo na maandiko yetu yanaendana na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya?
Sina shaka mtakubaliana nami kuwa bado tuko kule alipozungumzia Hayati Mzee Mkapa kwenye ujasiri wa maneno badala ya ujasiri wa kutenda. Bado baadhi yetu tunaopaswa kutekeleza hili tumeelemewa na kasumba ya kutoiamini Sekta Binafsi. Hatuna budi kutoka huko. Ndio sababu nimefurahishwa sana kuwa Kumbukizi hii imetukumbusha wajibu wetu na umuhimu wa ushupavu wa uongozi katika kuyafanikisha mabadiliko hayo. Kwa sasa, serikali yetu imejipambanua wazi wazi kushirikiana na Sekta binafsi kwa tija, kimkakati na kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Huwa nayasema haya kila ninapopata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara na wawekezaji ndani au nje ya nchi.
Kwa ajili hiyo, nitafurahi sana kupokea majumuisho yatokanayo na mjadala mliokuwa nao jana ili kwa pamoja tuyafanyie kazi. Nina taarifa kwamba Mawaziri wa Afya, Makatibu Wakuu na wataalam mbalimbali wa pande zetu mbili za Muungano walikuwepo kwenye mjadala. Bila shaka, wameyasikia na kuyatilia maanani, na nategemea kuwaona wakiyatekeleza.
Kwa upande wa sekta binafsi, natarajia nao, wataitikia wito wetu na kutoa ushirikiano, na kwamba watazingatia kuwa afya ni stahili ya umma (public good) na si biashara. Hivyo, lazima mzingatie urari (balance) kati ya kupata faida kiasi na kuwekeza katika kutoa huduma endelevu (Sustainable Socially Responsible Investment); na kuwekeza pale kwenye mahitaji makubwa zaidi kwa maslahi ya umma. Daima tusipoteze lengo kuu ambalo ni kufikisha huduma bora ya afya, kwa wote, popote na kwa gharama inayohimilika.
Mheshimiwa Rais,
Wageni Waalikwa;
Mniruhusu sasa nijielekeze kwenye kuwapongeza Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa ushirikiano wake mkubwa inaoendelea kuipatia Serikali; hususan katika uimarishaji wa mifumo ya afya (Health System Strengthening) na zaidi kwenye suala la kuongeza wataalamu na watumishi katika sekta ya afya (Human Resources for Health). Huko ndiko ambapo bado tuna changamoto ya uhaba wa watumishi kwa zaidi ya asilimia (50%) wanaohitajika.
Kupitia Taasisi hii, kwa miaka 16 sasa, watumishi wa afya wa kada mbalimbali wapatao 10,041 wakiwemo kada za madaktari, wauguzi, matabibu, wafamasia na kadhalika; pamoja na wahudumu wa Afya ngazi ya jamii (Community Health Workers), wamesambazwa kote nchini. Watumishi hawa wameongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma bora za afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Rais,
Wageni Waalikwa;
Ninatambua kwamba Serikali za pande zote mbili, Bara na Zanzibar zimewekeza na zinaendelea kuwekeza katika miundombinu (health infrastructure) ya sekta ya afya. Hivyo, hatuna budi kutilia mkazo kwa usawa ule ule kuwekeza katika raslimali watu kwenye hospitali au vituo vya tiba vinavyojengwa na kukarabatiwa. Katika hili, kwa mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imeweza kutoa vibali vya ajira 9,262; na itaendelea kupunguza uhaba huo, kadri uwezo wa Serikali wa kuajiri unavyoimarika.
Hali kadhalika, maeneo mengi duniani, zikiwemo nchi za Bara la Afrika, zimewekeza pia katika mbinu zilizo nafuu (cost effective) za kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii (community health workers), na wameweza kupata matokeo chanya yanayopelekea kufikia malengo ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage) na lengo la tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya dunia (SDG 3), ikiwemo pia kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.
Nasi kupitia Mikakati na Miongozo ya kitaifa na kisekta, tumekwishabainisha umuhimu wa kuwekeza katika Raslimali watu wa Sekta ya afya kwenye jamii na vituoni, Wito wangu ni kwa wanaosimamia masuala ya raslimali watu katika sekta ya afya, kutoa kipaumbele zaidi katika kuharakisha utekelezaji wa mikakati ambayo tayari imeshabainishwa kutatua changamoto hii. Aidha ushirikiano wa Serikali na Asasi za kiraia zikiwemo Taasisi ya Mkapa na Sekta binafsi pamoja na Wadau wa Maendeleo, uendelee kuimarishwa katika eneo hili la raslimali watu, kwa nia ya kuweza kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ifikapo mwaka 2030.
Nirudie kwamba Taasisi ya Mkapa mmeendelea kuwa wabia wazuri wa Serikali na mmetuunga mkono siku zote. Hivyo nataka kuwahakikishieni kuwa tunaufurahia ushirikiano wetu huu adhimu, na tunaahidi kuuendeleza sababu una tija kwa pande zetu mbili.
Nawapongeza pia kwa hatua mnayopiga katika kupunguza utegemezi na kujitegemea siku za usoni. Mwaka jana nilizindua Mfuko wa Wakfu (Endowment Fund) wa Taasisi hii. Naendelea kufarijika kwamba mfuko huu unajikita katika kuimarisha zaidi mipango ya kimkakati ya sekta ya afya, na pia kuhakikisha kuwa mchango wa Taasisi hii katika maendeleo ya sekta ya afya unakua endelevu.
Mwaka jana niliahidi kuchangia, na tayari nimeshachangia. Nimefurahi kusikia kuwa Mfuko huu umeshafikisha takriban kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni moja (1,000,000,000). Aidha, nimeambiwa kuwa jana chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Msarifu wa Mfuko huu, mliweza kuutunisha zaidi. Hongereni! Nawatia shime wengine wote kuunga mkono jitihada hizi na kuendelea kuuchangia Mfuko huu.
Sambamba na hilo, kilichonivutia zaidi pia ni mpango wenu wa kujenga jengo la Kitega Uchumi la âMkapa Health Plazaâ katika eneo la Kawe, Dar Es Salaam. Huu ni mkakati mzuri na ninawatakia kila la kheri. Hayati Mzee Mkapa aliamini sana katika kujitegemea. Nafarijika kuona kuwa imani yake hiyo mmeishika barabara.
Mheshimiwa Rais,
Waheshimiwa Viongozi, na
Wageni Waalikwa;
Kabla sijahitimisha, nimpongeze Mama Anne Mkapa. Ninafurahi kukuona ukiwa imara. Wiki mbili zilizopita Mama Mkapa alinipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (Equal Opportunity for All Trust Fund-EOTF). Nilitumia fursa ile kumshukuru hadharani kwa kunihimiza kugombea nafasi ya kisiasa na ikawa ndio mwanzo wa kuingia kwenye siasa. Na nilipoingia, Mzee Mkapa naye hakunitupa. Kwa hiyo, kwa ujumla naweza kusema, familia hii imechangia sana katika malezi na ukuaji wangu kisiasa. Nikuhakikishie kuwa tutaendelea kuwatunza na kuwaenzi kwa mchango wenu mkubwa katika nchi hii.
Hayati Mzee Mkapa hayuko nasi tena kimwili lakini amebaki nasi kifikra. Tunaendelea kufaidika na mchango wake mkubwa kwa Taifa letu. Tunaendelea kuvuna hazina ya hekima na uongozi wake. Hakika, alitimiza wajibu wake hapa duniani. Tuliobaki hatuna jengine zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya Hayati Benjamin Mkapa kwetu. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema, peponi, apumzike kwa Amani !
Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza!
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAâĶ!
