
Dakika 60 na Dk. Ellen, mwanamke wa kwanza kuiongoza Taasisi ya Mkapa
Na WILLIAM SHECHAMBO
KATIKA orodha ya Taasisi zenye jina kubwa nchini kwa sasa, huwezi kuiacha Taasisi ya Benjamin Mkapa (Benjamin William Mkapa Foundation - BMF), ambayo hadi leo tangu ilipoanzishwa miaka 16 iliyopita na Hayati Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa imefanikiwa kuwafikia watu zaidi ya milioni 26 kutokana na utekelezaji wa miradi yake mbalimbali ya afya.
Taasisi hii isiyo ya kiserikali na yenye sifa lukuki ndani na nje ya nchi, inaongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu mwanamke, Dk. Ellen Mkondya-Senkoro, ambaye gazeti hili mahususi kwa wanawake nchini, limefanikiwa kumpata na kuzungumza naye kwa dakika 60 kuhusu masuala kadha wa kadha katika mtindo wa maswali na majibu.
Mwandishi: Mafanikio ya Benjamin Mkapa Foundation yametokana na nini?
Dk. Ellen: Kwanza mafanikio makubwa yanatokana na mwanzilishi wake kwa maana ya Mhe. Hayati Mzee Mkapa, dira yake kubwa ilikuwa ni kuona jinsi gani anasaidia wananchi ambao labda wana changamoto ya kupata huduma bora kwa urahisi zaidi, kwahiyo nadhani ile ‘vision’ (dira) aliyokuwa nayo ya kufikia Watanzania wengi kwa ubora wa huduma pia wakiwa na afya njema na ustawi mzuri, ndiyo kigezo kikubwa cha mafanikio ya hii Taasisi.
Alipoanzisha hii taasisi, tafsiri ya dira yake ikaenda kuandikishwa na kutengenezewa mkakati wa miaka mitano, kwahiyo tulivyotengeneza huu mkakati ilikuwa inatusaidia kiuhalisia kujua nini kifanyike, na hivyo kuanzisha program mbalimbali zinazowafikia walengwa nchini. Kwa sasa tunatekeleza Mpango mkakati wa Taasisi wa awamu ya tatu ( Julai 2019- June 2024).
Jambo lingine, linalotupa mafanikio ni uwepo wa utawala bora, uongozi na utendaji imara bora unaosimamiwa na Bodi na Menejimenti makini tangu tulipoanzishwa. Pia tunajivunia kuwa ni taasisi ya Kitanzania, iliyoanzishwa na Mtanzania inaendeshwa na Watanzania na inawatumikia Watanzania Bara na Visiwani, tuna ubunifu, tuna watendaji wenye sifa na weledi u na tunaaminiwa na Serikali na wafadhili.
Mwandishi: Unajisikiaje kuwa kiongozi mwanamke unayeongoza taasisi hii nyeti iliyobeba jina lenye sifa lukuki nchini, kikanda na kimataifa?
Dk. Ellen: Ninajisikia vizuri, lakini kikubwa ninaamini matokeo yanayopatikana sio tu kutokana na uongozi wangu pekee yangu, bali ni kutokana na uwepo wa watendaji wenye sifa na weledi, na pia mashirikiano na wadau mbalimbali. Kwangu ninpopata matokeo yaliyokusudiwa ndio ninafarijika zaidi na hasa kama unafikia malengo mliyojiwekea kama taasisi. sisi hapa tuna utaratibu wa kujipima kila mwaka kama Taasisi na pia kama Afisa Mtendaji Mkuu na Menejimenti yote tunapimwa utendaji na bodi, na vilevile kwa kila mtumishi kadhalika.
Unajua unaposimamia taasisi iliyobeba jina la Rais Mkapa, yeye mwenyewe alikuwa ni kiongozi mchapakazi, mtu anayependa kuona matokeo, asiye na maneno mengi, yaani ni mtu ambaye alikuwa anajiamini na mwenye kutahmini uadilifu.
Kwahiyo nilivyopewa hii taasisi, nilivyoanza, na mimi ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kwanza wa hii taasisi tangu ilipoanza, ilibidi mimi mwenyewe nijipime kama ninatosha katika hii nafasi na ninaendana na sifa za Rais Mkapa katika kufanya kazi.Nilipoona ninaweza kukidhi haja, basi ilikuwa ni rahisi kufanya kazi na nafikiri ni sehemu niliyojifunza sana kama kiongozi, kuna maeneo mengi nimekomaa nikiwa hapa.
Mwandishi: Baadhi ya wanawake ni waoga wanapopata nafasi nyeti kama hii, lakini wewe umethubutu na unafanya kazi kwa weledi nini siri iliyopo nyuma ya mafanikio haya?
Dk. Ellen: Hii sio mara yangu ya kwanza kufanya kazi kama kiongozi, hata nilikotoka niliwahi kushika nafasi ya uiongozi kama ‘DMO’ (Mganga Mkuu wa Wilaya Temeke na Kinondoni). Mimi nimesoma zaidi hapa Tanzania kuanzia sekondari, nikasoma Chuo Kikuu cha Muhimbili Digrii ya Udaktari, na nilipomaliza nikaenda kusoma Masters degree ya Public Health Uholanzi, nilivyorudi nikapangiwa kazi serikalini. Baada ya hapo
nilikwenda kufanya kazi Umoja wa Mataifa,Ofisi ya Dar Es Salaam na baadaye ndio nikaja hapa. Kote nilikopita kufanya kazi nilijengwa sana na viongozi wangu na utayari wangu wa kujifunza ndio ilikuwa siri yangu kubwa. Kwahiyo hatua hiyo kidogo ilinijenga lakini pia kikubwa kwangu ni kujiamini, kuwa tayari kutumia watu, makuuzi na malezi ya wazazi wangu, na pia kuungwa mkono na walio karibu namiwakiwemo wana familia.
Mwandishi: Una maoni gani kwa wanawake katika ushiriki wa ujenzi wa taifa ili kukuza uchumi?
Dk. Ellen: Wanawake wana fursa nyingi na wanajituma na kuchangia kiasi kikubwa katika kukuza uchumi. Aidha pia serikali yetu imekuwa mstari wa mbele kuwatambua na kuwawezesha wanawake, na sasa hivi tumeweka historia duniani, tuna Rais mwanamke ambaye tunaamini yeye ndiye kinara wetu wa kutusogeza mbali zaidi, kama nchi.
Tumeona hata kwenye teuzi katika Serikali na Taasisi mbalimbali, wanawake wanashika nafasi za uongozi, na pia hata kwenye ngazi ya familia, wanawake wana nafasi kubwa ya kukuza uchumi kutokana na shughuli zao mbalimbali.Hata hivyo bado tunahitaji kujiamini na kuongezeka zaidi kwa wanawake katika safu za uongozi, zikiwemo pia Bodi au vyombo vya kufanyia maamuzi katika Serikali, Taasisi za Umma na za binafsi.