Kada Ya Afya Mwanza, Simiyu Kunufaika
Na Damian Masyenene, Mwananchi dmasyenene@mwananchi.co.tz
Mwanza. Taasisi ya Benjamim Mkapa imepanga kutoa fursa za ajira za kujitolea kwa wataalam 151 wa sekta ya afya katika Mikoa ya Mwanza na Simiyu.
Ajira hizo ni utekelezaji wa muongozo wa Taifa wa ajira katika kada ya afya unaolenga kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi maeneo ya pembezoni.
Akizungumza jijini hapa jana Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Hellen Senkoro alisema kupitia muongoso huo unaowawezesha wa hitimu wa kada za afya wasio na ajira rasmi kupata ajira za muda, Mkoa wa Mwanza utapata wataalamu wakujitolea 80, huku wengine 71 wakienda mkoa wa Simiyu.
Alisema Pamoja na kulipiwa bima ya afya kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya afya(NHIF) na michango kwenye mifuko ya jamii,wanufaika wa mpango huo pia watalipwa posho inayolingana, nusu au asilimia 50 ya mishahara wanayolipwa wataalamu wenzao walioko katika ajira rasmi.
Kwa upande wa Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mwanza (Mipango na Uratibu) Joachim Otaru alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wengine kuongeza ubunifu wa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Boniface Richard aliahidi kuwa ofisi yake itawaandalia mazingira bora ya kazi wataalamu wa kujitolea watakaopelekwa mkoani humo, na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano wa taasisi ya Mkapa kwa kusaidia kupunguza uhaba wa wataalamu wa afya hasa maeneo ya vijijini.