Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na wafanyakazi wa Mkapa Foundation tunapenda kutoa shukrani kwa ushirikiano endelevu wa Taasisi yetu na Serikali kwa miaka 14 tokea tulipanzishwa.
Hakika tumefanya kazi kubwa yenye matokeo chanya kwa ushirikiano katika kuimairisha mifumo ya sekta ya afya ikiwemo miundo mbinu na masuala ya wataalam wa afya katika vituo vya tiba na pia kwenye jamii.
Taasisi ya BMF kwa miaka 14 yote tokea mwaka 2006 hadi Desemba 2019, tumeshaweza kutoa ajira za wataalam wa afya 2181 ambao wamekuwa wakitoa huduma katika Hospitali na Vituo vya tiba nchini kote, hususan vituo vya serikali na baadhi kwenye vituo vya kidini.
Tumeweza kutekeleza haya yote kwa kupitia fedha za wafadhili mbalimbali wakiwemo Global Fund, Irish Aid, Serikali ya Norway na Abbott Fund.
Kwa leo hii tunafarijika tena kuwa sehemu ya mikakati ya kitaifa ya kuimarisha huduma za ukimwi, kifua kikuu na malaria pamoja na magonjwa ya milipuko kama COVID 19 na hivyo kuchangia tena katika kupeleka watalaam wa afya 307 katika Halmashauri 68 (mIkoa 11) na wiki ijayo tutamalizia usaili wa kuwapeleka wataalam wa afya 80 kwenye hospitali za rufaa nchini.
Taasisi yetu inaamini kwenye ubunifu, ufanisi na matokeo makubwa ya haraka na hivyo kwa nafasi hii tunapenda kuishukuru Serikali ya Tanzania na kuwaomba iendelee na ushirikiano wa aina hii na asasi zisizo za kiraia ikiwemo na ya kwetu ya BMF, katika kuleta maendeleo yanayooonekana dhahiri na yenye kumnufaisha mwananchi haswa anayeishi katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi ( kama vijijini).
Tunapenda kuwahakikishia watanzania wote kwamba Taasisi yetu ya BMF tutaendelea kutoa ushirikiano mkubwa na kuwa mstari wa mbele katika pia kupambana na hili janga la CORONA kupitia miradi yetu yote ambayo imeweka wataalam wa afya vituoni na pia wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Asanteni.
Imeandaliwa na
AFISA MTENDAJI MKUU , BENJAMIN WILLIAM
MKAPA FOUNDATION