Serikali, Wadau kushirikiana kukabiliana Uhaba wa Watumishi Sekta ya Afya

Serikali imesema itaendelea kushirikisha sekta binafsi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya ili kukabiliana na tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya toka TAMISEMI Dkt. Ntuli Kaporogwe
leo alhamisi Novemba 18, 2021 kwenye mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika watumishi kwa lengo la kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto wakati wa Mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi, mtoto, vijana na lishe unaoratibiwa na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete kwa kushirikiana na Wizara ya Afya unaofanyika jijini Dar es salaam.
Akitoa maelezo kuhusu namna serikali kupitia TAMISEMI inavyosimamia utoaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri Dkt. Kapologwe amesema, Serikali bado inakabiliwa na uhaba wa watumishi katika sekta ya afya jambo ambalo linahitaji ushirikishwaji wa sekta binafisi ili kuendelea kuimarisha utoaji huduma.
“Bado tunatatizo la vifo vitokanavyo na uzazi. Ukiangalia takwimu ni kwamba takribani 90% ya vifo vinavyotokana na uzazi vinatokea katika vituo vyetu vya kutolea huduma kwa sababu ya uhaba wa watumishi na pia waliopo baadhi yao hawana umahili na ujuzi wa kukabiliana na matatizo haya.” Alisema Dr. Ntuli.
Akieleza mipango ya Serikali kukabiliana na tatizo hilo, Dr. Ntuli amesema tayari Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau walizindua mwongozo wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline) kama sehemu ya mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya nchini.
“Pamoja na mwongozo huu ambao tutaendelea kuutekeleza hivi karibuni, tunawashukuru wadau kutoka sekta binafsi kama vile Mkapa Foundation, MDH, Amref na wengine ambao wamekuwa wakiwekeza katika eneo hili kwa kuajiri watumishi wa afya kwa miongozo ya Serikali na kuwapeleka katika vituo vya Serikali katika Halmashauri zetu.” Aliongeza Dkt. Ntuli
Awali akitoa uzoefu wa utekelezaji wa afua za upatikanaji wa watumishi wa afya kupitia sekta binafsi, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa, Rahel Sheiza alisema kulingana na takwimu zilizopo wadau kutoka sekta Binafsi (NSAs) wanachangia zaidi ya ajira 3,000 za watumishi kila mwaka katika sekta ya Afya wanaochangia utoaji wa huduma bora za Mama, Mtoto, Baba na Vijana.
Pamoja na jitihada hizo kutoka kwa wadau, bado mchango huo wa watumishi wanao ajiriwa na wadau mbalimbali katika sekta ya Afya hauakisiwi katika taarifa za idadi ya watumishi nchini, hivyo ni dhahiri kuwa pengo lililopo hivi sasa la 52% linaweza kuwa chini zaidi kama mchango wa wadau utajumuishwa katika taarifa za watumishi.
“Ukosefu wa takwimu hizi hususani katika kuainisha upungufu wa watumishi wanaohitajika na waliopo kwenye sekta ya afya hapa nchini unasababisha pia kutokuwa na mipango thabiti katika Nchi. Kwa mfano Mkapa Foundation pekee tumeajiri watumishi 1263 katika Halmashauri 161 Nchini wanaotoa huduma za Afya ya Mama na Mtoto katika ngazi zote za vituo vya huduma za Afya. Hawa wakiingizwa katika takwimu za kitaifa upungufu huo unaweza kuwa chini kidogo. Alisema Bi. Sheiza
Akizingumzia kuhusu mwongozo wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline), Bi. Sheiza amesema Taasisi ya Mkapa inaamini kuwa utekelezaji wa mpango huu katika ngazi za vituo vya huduma za Afya ni moja kati ya njia itakayosaidia kupunguza changamoto ya watumishi katika vituo vya huduma za Afya kabla ya Ajira rasmi kutolewa na Serikali.
“Sisi Mkapa Foundation tumeshiriki katika kila hatua wakati wote wa kuandaa mwongozo huu na mpaka unazinduliwa, endapo Serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya Afya watausimamia utekelezwe kama unavyokusudia, utaleta matokeo chanya hususani katika utoaji huduma za Afya ya Mama na Mtoto kwa kuwa watumishi wakutosha watakuwepo katika vituo vya kutolea huduma. Aliongeza Bi. Sheiza.
Nae Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Dr. Maneno Focus akichangia mdahalo huo, amesema ipo haja ya serikali hususani TAMISEMI kuja na mkakati maalumu wa utekelezaji wa mwongozo huu ili Halmashauri zote ziweze kunufaika na uwepo wake.
“Tunaitaji mpango harakishi utakaotuwezesha tuanze kutumia watumishi wa kujitolea ili tuendelee kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Hawa watumishi wapo, ni swala la kujipanga hususani kupitia mapato ya ndani ili tuweze kuimarisha utoaji huduma. Alisema Dkt. Focus