Dr. Hussein Ali Mwinyi is the President of Zanzibar, also the First Chair of the Benjamin William Mkapa Foundation Board of Trustees
14th July, 2021
Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marais Wastaafu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Marais wengine Wastaafu Marafiki wa Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa;
Mama Anna Mkapa, Mjane wa Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Wanafamilia;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mwenyeji wetu, Mheshimiwa Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa mliopo;
Dkt. Adeline Kimambo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa;
Dkt. Ellen Mkondya Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisiya Benjamin Williiam Mkapa;
Viongozi wengine wa Serikali mliopo;
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo; Viongozi wa Asasi mbalimbali za Kiraia;
Wageni Waalikwa, Wana-Habari, Mabibi na Mabwana:
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Siku zote ni vigumu sana kuzungumza baada ya wazee ambao wanaifahamu vyema mada husika. Nimewasikiliza kwa makini wote waliomzungumzia Hayati Rais Mstaafu Mzee Mkapa. Ni watu wenye kumfahamu na wamefanya naye kazi kwa karibu zaidi. Kwa hiyo, wamezungumza yote kuhusu Mzee Mkapa. Kwa kifupi, wamemwelezea Mzee Mkapa kuwa Kiongozi aliyekuwa na maono makubwa, jasiri, shupavu, imara, mpenda maendeleo, mwana diplomasia nguli, mwenye kutaka kuona matokeo, na mtetezi wa walionyimwa haki.
Nakubaliana na hayo yote. Mimi pia nimebahatika kumfahamu Hayati Rais Mkapa. Naweza kuthibitisha kuwa yote yaliyosemwa na walionitangulia kuzungumza ni ya kweli. Mzee Mkapa alikuwa mtu wa kipekee sana. Mara zote, ilikuwa ukipata fursa ya kukutana na kuzungumza naye, utaondoka ukiwa umevuna mambo mengi. Hakuwa mchoyo wa maarifa au taarifa anazozijua. Alikuwa mtu mwenye haiba ya mamlaka na kujiamini. Alikuwa mwenye ufahamu mkubwa na busara nyingi; na hiyo imejidhihirisha kwenye maandiko yake mengi.
Kwa hakika, yaliyoelezwa hapa yanathibitisha umuhimu wa kuandaliwa kwa Kongamano hili. Hivyo basi, naishukuru na kuipongeza Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa maandalizi mazuri ya Kongamano hili na kunialika. Kabla ya kuingia Ukumbini, nimepata fursa ya kutembelea Mabanda ya Maonesho ya Kazi za Taasisi hapo nje. Nimefurahi sana kuona jinsi Taasisi inavyojitahidi kuendeleza kazi nzuri iliyoasisiwa na Mzee Mkapa. Nawasihi wote mliopo Ukumbuni, na wale wanaonisikiliza, kutafuta muda wa kutembelea Mabanda hayo ili kujionea wenyewe kazi nzuri inayofanywa na Taasisi hii, kwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Adeline Kimambo na Afisa Mtendaji Mkuu Dkt. Ellen Senkoro; ambao wote ni wanawake. Na hii inathibitisha kuwa, wanawake ukiwakabidhi jambo haliharibiki.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Nina uhakika nitakuwa sijaongeza chumvi nikisema, Kitabu cha Historia ya Taifa letu hakiwezi kukamilika bila ya kuwepo kwa Sura nzima itakayomwelezea Hayati Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Na hii sio tu kwa sababu Mzee Mkapa alikuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa nchi yetu bali pia kutokana na mageuzi makubwa aliyoifanyia nchi yetu.
Sote tunafahamu, jinsi ambavyo, wakati wa Uongozi wake, Mzee Mkapa alisimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini. Miongoni mwa hatua kubwa alizochukua ni kutoa fursa kubwa zaidi kwa sekta binafsi na kukaribisha uwekezaji kutoka nje. Hatua hizi zilisaidia kuongeza mapato ya Serikali kutoka shilingi bilioni 331.2 mwaka 1995 hadi kufikia shilingi trilioni 2 mwaka 2005. Aidha, Mzee Mkapa alifanikiwa kupunguza deni la taifa kwa zaidi ya asilimia 50, kutoka asilimia 143.7 ya Pato la Taifa mwaka 1995 hadi asilimia 60.7 mwaka 2005. Na hii iliwezekana baada ya Mzee Mkapa, kwa kutumia uzoefu wake wa diplomasia, kuzishawishi taasisi za kifedha za kimataifa na nchi wahisani kuisamehe madeni iliyodaiwa nchi yetu kupitia Mpango wa HIPC uliosimamiwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF). Hii pia ilisaidia nchi wahisani na taasisi za kifedha za kimataifa kurejesha uhusiano na nchi yetu na hivyo kuanza tena kutupatia mikopo na misaada.
Vilevile, Mzee Mkapa ataendelea kukumbukwa kwa kujenga mifumo imara ya kitaasisi ya Serikali. Miongoni mwa taasisi zilizoanzishwa kipindi cha Mzee Mkapa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Mfuko wa Kusaidia Masikini (TASAF); Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mpango wa Kurasimisha Mali (MKURABITA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Tume ya Kupambana na UKIMWI (TACAIDS). Taasisi hizi mpaka leo zipo na zinaendelea kutoa huduma na kuchochea ukuaji uchumi wa nchi yetu.
Ni katika kipindi cha Mzee Mkapa pia ndipo Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini (MKUKUTA), Sera Mpya ya Mambo ya Nje pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2000 – 2025 ilipitishwa. Hii inaonesha kuwa, mbali na kuangalia matatizo ya wakati huo, Mzee Mkapa alikuwa pia ana maono ya kuangalia mustakabali wa nchi kwa nyakati za mbele zaidi.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Mchango wa Mzee Mkapa haukuishia kwenye mipaka ya nchi yetu bali pia nje ya Tanzania. Alishiriki kikamilifu katika kuifufua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akichukua kijiti kutoka kwa Mzee Mwinyi. Aidha, alitoa mchango wake wakati wa kugeuza uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kuwa Umoja wa Afrika (2001) na halikadhalika, kwenye mchakato wa kutafuta amani wa Burundi uliopelekea Kusainiwa kwa Mkataba wa Amani na Maridhiano wa Burundi mwaka 2000.
Zaidi ya hapo, Mzee Mkapa alitoa mchango mkubwa kwenye Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Gaborone nchini Botswana. Wakati akikabidhi Uenyekiti wa SADC mwaka 2004, baada ya kuona wafadhili wanasuasua, Mzee Mkapa alitoa wito kwa Nchi Wanachama kutoa michango kuanza ujenzi wa Ofisi hiyo. Wazo hilo liliungwa mkono na Nchi zote Wanachama. Katika hilo, alitangaza kuwa Tanzania ingechangia Dola za Marekani 500,000.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Sambamba na hayo, sifa nyingine kubwa ya Mzee Mkapa ni uwezo wake mkubwa wa kuhimili ama kutoogopa mijadala ya kimataifa. Na hapa kuna mifano mingi. Sote tunakumbuka, kwenye miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka 2000, kulikuwa na vuguvugu kubwa la kupinga masuala ya Utandawazi; na baadhi ya watu, wakiwemo baadhi ya viongozi walitumia fursa hiyo kujipatia umaarufu. Mzee Mkapa yeye akufuata mkumbo. Badala yake, alijitokeza hadharani kutetea Utawandazi na kueleza kwanini tunapaswa kuupokea. Na katika hili, alifanya kazi kubwa mbili. Kwanza, kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Utandawazi; na pili, kutumia uzoefu wake kidiplomasia, kuieleza dunia kuhusu umuhimu wa kuwa na Utandawazi unaojali maslahi ya makundi yote.
Hii ndiyo ilipelekea Mzee Mkapa akateuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Tume iliyoundwa na Shirika la Kazi Duniani ya Kushughulikia Masuala ya Utandawazi (ILO Commission on Social Dimension of Globalization), akishirikiana na Mheshimiwa Tarja Halonen, aliyekuwa Rais wa Finland. Aidha, kama alivyoeleza, tulivyomsikia Mheshimiwa Tony Blair, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, alikuwa Mwenyekiti Mwenza na Mzee Mkapa kwenye Kamisheni kuhusu Masuala ya Afrika (Commission for Africa). Zaidi ya hapo, Mzee Mkapa alikuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya kushughulikia Masuala ya Nchi Zinazoendelea (South Commission). Kupitia ushiriki wa Mzee Mkapa kwenye vyombo hivyo, sauti ya Afrika na nchi zinazoendelea iliweza kusikika.
Lakini niseme, mimi binafsi pia nimewahi kuushuhudia uwezo wa Mzee Mkapa kwenye masuala ya kimataifa. Nakumbuka, mwaka 2001, baada ya kutokea kwa machafuko kule Zanzibar, Mzee Mkapa aliniteua pamoja na Rais Mstaafu, kaka yangu, Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais mstaafu wa Zanzibar Mhe. Ali Mohamed Sheni kwenda nchi mbalimbali kuelezea kilichotokea Zanzibar na hatua ambazo nchi imepanga kuzichukua. Katika kuifanya kazi hiyo, nilijifunza mambo mengi ya siasa na diplomasia pamoja na hekima ambayo Wakuu wa Nchi wanapaswa kutumia kunapotokea changamoto hasa za kisiasa. Hatua hii ndiyo iliyoleta muafaka wa kisiasa Zanzibar na nchi kwa ujumla kuendelea na shughuli zake bila vikwazo vya ndani walaVya kimataifa.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Baada ya kustaafu, Mzee Mkapa hakupumzika, aliendelea kujishughulisha na masuala mbalimbali ya Kikanda, Barani Afrika na Kimataifa. Sote tunakumbuka, wakati mauti yanamkuta, Mzee Mkapa alikuwa Msuluhishi wa Mgogoro nchini Burundi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi wa Afrika (the African Leadership Forum). Nimefurahi kuona kuwa viongozi wenzake wa Jukwaa hilo, akiwemo Rais Mstaafu, Olesegun Obasanjo wanafuatilia Kongamano hili kwa Njia ya Mtandao.
Ndani ya nchi Rais Mstaafu Mkapa aliendelea kutoa mchango wake kupitia Taasisi aliyoianzisha. Taasisi hii inatoa mchango mkubwa kwa nchi yetu, hususan katika sekta ya afya. Kama ilivyoelezwa hapa kwamba, mbali na mambo mengine, Taasisi imeweza kuajiri wataalam wa afya 3,760, kujenga nyumba za watumishi wa afya 482 na kutoa ufadhili wa masomo ya afya kwa wanafunzi 933.
Kwenye Kitabu cha Wasifu wake, Mzee Mkapa amekiri kuwa wazo la kuanzisha Taasisi ya Benjamin William Mkapa alilipata kutoka kwa Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton. Hivyo basi, mniruhusu kutumia jukwaa hili kumshukuru na kumpongeza Rais Mstaafu Clinton kwa kumshawishi Hayati Mzee Mkapa kutekeleza wazo hilo. Nina taarifa kwamba, Mheshimiwa Clinton naye anashiriki Kongamano hili kwa njia ya mtandao. Ahsante sana.
Aidha, kwa namna ya pekee, nawashukuru na kuwapongeza wadau na wahisani wote ambao wamekuwa wakiunga mkono kazi zinazofanywa na Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 198 hadi kufikia mwezi Juni, 2021. Nawasihi mwendelee kuiunga mkono Taasisi hii.
Na katika hilo, nitumie fursa hii kuipongeza Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa kubuni wazo la kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji (Endowment Fund). Hili ni wazo zuri, ambalo sio tu litatoa uhakika wa Taasisi kuendelea na kazi zake, bali pia linaendana na msimamo wa Mzee Mkapa kuhusu umuhimu wa kujitegemea. Kwa msingi huo, Serikali inaunga mkono kuanzishwa kwa Mfuko huo na ni ahadi yangu kwamba Serikali itachangia. Nawasihi wadau wengine nao kuchangia ili kuukuza Mfuko huu.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Muda mfupi uliopita, umefanyika Mjadala wenye kaulimbiu “Huduma za Afya kwa Wote: Urithi wa Rais Benjamin William Mkapa katika kujenga Mifumo Imara ya Sekta ya Afya”. Mjadala huu ni muafaka na umefanyika kipindi sahihi. Hayati Rais Mkapa alikuwa muumini mzuri wa masuala ya afya kwa wote. Kwa upande mwingine, kama mnavyofahamu, hivi sasa Serikali ipo kwenye mchakato wa Mfumo wa Kutoa Huduma za Bima ya Afya kwa wote. Na kwa sababu hiyo, nimefurahishwa sana na Majadiliano yaliyofanyika. Nina uhakika, endapo wataalam wetu wa afya, wakiyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kuyatekeleza, yatasaidia sio tu katika kuharakisha kufikia utoaji huduma za afya kwa wote, lakini pia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini. Na hapa nataka niwe mkweli, binafsi, natamani na kwa hakika nitafurahi sana, endapo majadiliano yaliyofanyika, yatatuwezesha kuboresha huduma za Afya ya Uzazi na Afya ya Mtoto kwa kuwa masuala haya ni ajenda ya moyoni mwangu.
Lakini, sambamba na hayo, naamini, majadiliano yaliyofanyika yatatuwezesha kukabiliana na changamoto nyingine za afya zinazokabili nchi yetu na dunia kwa ujumla, ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19. Kuhusu janga hili la UVIKO-19, Serikali inaendelea kumtaka kila mwananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa kwa kufuata maelekezo ya wataalam wetu wa afya kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Kwa upande mwingine, Serikali tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kakabiliana na ugonjwa huu, ambapo kwa sasa tunakamiilisha taratibu za kuagiza chanjo kwa ajili ya kinga. Mwelekeo ni kwamba kila atakayehitaji huduma ya chanjo hiyo iwe inapatikana. Kama nilivyosema awali, kuwa chanjo hiyo ni ya hiari; hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwaomba wadau wa afya kuunga mkono jitihada hizo za Serikali.
Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;
Nimehakikishiwa kuwa Kongamano hili litakuwa linafanyika kila mwaka. Kwa sababu hiyo, haitakuwa vyema kumaliza kueleza yote yanayomhusu Mzee Mkapa hasa kwa kuwa Mzee huyu tulimfahamu kama Kiongozi wa Serikali na vilevile Kiongozi wa Kisiasa. Hivyo, kwa leo, ningependa niishie hapa.
Hata hivyo, kabla sijahitimisha napenda kurudia kuishukuru Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa kuandaa Kongamano hili la Kumbukizi ya Maisha ya Hayati Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Nataka niwahakikishie kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano uliopo, ikiwemo katika kutekeleza Mpango Mkakati wenu wa Tano wa Afya utakaotekelezwa katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo, ambao mmeuzindua hivi karibuni. Kwa bahati nzuri yote yaliyomo kwenye Mpango Mkakati wenu, yamo pia kwenye Mpango wetu wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Kwa Mama yetu Anna Mkapa pamoja na familia, nataka niwahakikishie kuwa Serikali ipo na itakuwa pamoja nanyi kwa kila hali. Na hapa nataka niwape taarifa ndugu washiriki wa Kongamano hili kuwa mimi nimebahatika kulelewa na wote, Mzee Mkapa (akiwa Kiongozi kwenye Serikali – Kazi/Vijana na Wanawake) na Mama Mkapa (EOTF – alinipa ujasiri wa kuingia kwenye shughuli za kisiasa). Kwa marafiki, wahisani na wadau wetu wa maendeleo; nawasihi mwendelee kushirikiana nasi na kuiunga mkono Taasisi ya Benjamin William Mkapa ili iendelee kuwahudumia mamilioni ya Watanzania. Nimefurahi na kupata moyo kuona Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wakuu na Wawakilishi wa Taasisi, Mashirika na Kampuni wenyeji na wale wa kimataifa mko hapa pamoja nasi. Hii ni kuonesha jinsi mnavyoithamini taasisi hii.
Mabibi na Mabwana; napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kutumia maneno ya aliyekuwa Kiongozi wa India, Mahatma Gandi ambaye aliwahi kusema, nanukuu “Great men never die, and it is up to us to keep them immortal by continuing the work they have commenced” akimaanisha kuwa “Watu au Viongozi Mahiri huwa hawafi na ni juu yetu kuwahuisha/kuwafanya waendelee kuishi kwa kuendeleza kazi walizozianzisha”. Kwa hiyo, niwasihi ndugu zangu twende kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na Mzee wetu.
Serikali huwa tuna ahadi yetu ya kuyatunza na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Viongozi wa Awamu zote zilizotangulia na kuleta mema mapya. Na katika hilo, tunatambua kuwa, viatu vyao ni vikubwa, lakini tutajitahidi, ikibidi, tutaweka na sponji au kuongeza soksi.
“AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA”
Speech-Rais-wa-Zanzibar-on-Mkapa-Legacy-