TAASISI YA BENJAMIN MKAPA YATOA MSAADA WA VIFAA KINGA

Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) imetoa msaada wa vifaa kinga katika halmashauri mbalimbali na maeneo ya mipakani ya kanda ya Kaskazini vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 155. Vifaa hiyvo vinalenga kuongeza nguvu na jitihada za serikali katika mapambano dhdi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Afisa wa mradi kanda ya kaskazini wa Taasisi hiyo bwana Ponjoli Kabepele aliiambia Nipashe kuwa misaada ya vifaa hivyo imetolewa katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kupitia ufadhili wa UNFPA Tanzania. “Kimsingi maeneo yaliyolengwa kwenye ugawaji huu ni mipaka ya Namanga mkoani Arusha, Holili mkoani Kilimanjaro na Horohoro mkoani Tanga. Pia tumevilenga viwanja vya ndege, hasa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), uwanja wa ndege wa Arusha na bandari ya Tanga” alisema Kabepele.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo lengo la kugawa vifaa hivyo ni kuzuia maambukizi kwenye maeneo hayo ambayo yanaingiza na kupokea wageni wengi kutoka nchi za nje. Aidha, alitaja vifaa vilivyogawiwa kuwa ni barakoa 168,600 na jozi 168,600 za gloves. Mkoa wa Arusha ulipata barakoa 72,000 na jozi za gloves 72,000, wakati Tanga walipokea barakoa 5,700 na jozi za gloves 5,700 na mkoa wa Kilimanjaro ulipata barakoa 90,900 na gloves 90,900.
Alisema lengo la Taasisi hiyo ni kuunga mkono Serikali, jamii na wadau kwa ujumla kwenye kuongeza jitihada za kupambana na Uviko-19, hasa katika kuchangia vifaa kinga, chanjo na pia elimu ya uhamasishaji wa chanjo.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga Dk. Wilson Ligoha ambaye ni Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo alisema vifaa hivyo vitaongeza nguvu kuhamasisha wataalamu wa afya wilayani hapo katika kampeni zinazoendelea za kupambana na maambukizi ya virusi vya uviko. Ligoha alisema pia msaada huo utaipunguzia serikali gharama ambazo ingezitumia na badala yake itazielekeza katika pande nyingine kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Nae Afisa Afya wa kituo cha afya cha Horohoro, Haruna Kimaro, alisema vifaa tiba walivyopokea vitasaidia kuwakinga na virusi vya UVIKO-19 watumishi wanaohusika kupokea na kupima wagonjwa. Afisa afya wa bandari ya Tanga Magesa Kusaga, alishukuru kwa msaada wa vifaa kinga ambavyo vitazuia maambukizi kutoka kwa wageni wanaotumia bandari kutoka nchi mbalimbali duniani kwenda kwa watumishi wa afya na kuenea sehemu nyingine.
