UNFPA na Taasisi ya Mkapa (BMF) zakabidhi jengo hospitali ya Amana, yatoa vifaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu duniani (UNFPA) limekabidhi jengo la wodi ya mama na watoto kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana pamoja na vifaa tiba mbalimbali vitakavyotumika katika hospitali hiyo.
UNFPA kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) walikuwa wakishirikiana katika kutekeleza mradi wa “Tokomeza Uviko-19” hasa kwa mama wajawazito kwa kuwapatia huduma bora za afya.
Akizungumzia mradi huo jana, Ofisa Miradi Mwandamizi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Daud Ole Mkopi alisema taasisi yake kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland pamoja na UNFPA wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali za afya ikiwemo kuongeza ajira.
Alisema katika mradi huo, wameajiri watumishi wa afya 209 ambao wametawanywa katika mikoa mbalimbali. Watumishi 77 kati ya hao, wameajiriwa kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Finland na 45 kati yao wamepangiwa vituo vya kazi katika mkoa wa Dar es Salaam.
“Tumekarabati majengo saba katika mikoa sita tofauti kwa ufadhili wa Serikali ya Finland ikiwemo jengo la wazazi katika hospitali ya Amana ambalo limegharimu Sh120,” alisema Dk Mkopi.
Mwakilishi wa UNFPA hapa nchini, Mark Schreiner alisema wanafanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba wanawake wanapata huduma bora za afya na kwamba mwanamke yoyote hatakiwi kupoteza maisha wakati analeta maisha ya kiumbe mwingine.
https://youtu.be/Jz0y1ox9aO8
“Jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kwamba wanawake katika maeneo ya vijijini wanapata huduma bora za afya ya uzazi na kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua,” alisema Schreiner.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwenye sense itakayofanyika nchini Agosti 23 kwa kile alichobainisha kwamba takwimu halisi itaisaidia serikali na wadau wengine katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Mfaume alisema katika kukabiliana na Uviko-19, mkoa wa Dar es Salaam ulianzisha mbinu malumu ya kuhamasisha wananchi kwenda kuchanja kupitia kwa viongozi wa serikali za mitaa.
“Mkoa wa Dar es Salaa tulianza kuwahamasisha viongozi wa serikali za mitaa ili nao wakahamasishe wananchi wao. Hili limepata mafanikio makubwa ndiyo maana maeneo mengine wakaanza kutumia model yetu,” alisema.
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Riita Swan alisema wameamua kugawa pia vizibao vya kuakisi mwanga (reflector) vyenye ujumbe wa kuhamasisha wananchi kwenda kuchanja, lengo likiwa ni kuongeza hamasa ya watu kuchanja.
Kama ilivyoandikwa na Peter Elias