HAYATI RAIS MSTAAFU WA AWAMU YATATU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BENJAMIN WILLIAM MKAPA

KUZALIWA

Rais Mstaafu  wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa alikuwa mtoto wa Mzee William Matwani na Mama Stephania Nambanga. Alizaliwa tarehe 12 Novemba,1938 katika Kijiji cha Lupaso kilichopo Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara akiwa ni mtoto wa mwisho wa familia yenye watoto wanne (4).

ELIMU

 • Hayati Benjamin William Mkapa alipata Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Lupaso na baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ndanda ambapo alisoma kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1948 hadi 1951 kisha alijiunga na Seminari ya Kigonsera Mkoani Ruvuma.
 • Alijiunga na Shule ya Mtakatifu Fransisco Pugu mwaka 1955 na kumaliza mwaka 1956 kwa ajili ya elimu ya kidato cha tano na sita.
 • Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kwa masomo ya Shahada ya kwanza kuanzia mwaka 1959 hadi mwaka 1962 alipohitimu na kupata Shahada ya Kwanza ya Fasihi ya Kiingereza na Fonetiki.
 • Mwaka 1963 alipata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Diplomasia ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Columbia, nchini Marekani.

KAZI KAMA AFISA WA KAWAIDA SERIKALINI

Hayati Benjamin William Mkapa alianza kazi kama Afisa Tawala Serikalini  Wilaya ya Dodoma, Mkoani Dodoma mwezi Aprili, 1962. Baada ya miezi minne  (4), mnamo Agosti, 1962 alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Diplomasia katika Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.

Aliporejea kutoka Masomoni mwaka 1963 alifanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje katika Dawati la Afrika akiwa na cheo cha Afisa wa Mambo ya Nje. Miongoni mwa kazi zake ilikuwa kuchukua muhtasari wa mazungumzo  ya Waziri wa Mambo ya Nje au Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania anapokuwa na wageni.

KAZI ZA UONGOZI

Hayati Benjamin William Mkapa alifanya kazi Serikalini kama Afisa wa kawaida kwa kipindi kifupi sana. Kwa sehemu kubwa ya Utumishi wake Serikalini, Hayati Mkapa alikuwa ni Kiongozi katika nyadhifa mbalimbali kama ifuatavyo:-

 • Mwaka 1966 aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Chama  Cha TANU (The Nationalist).  Kazi hii ilimuwezesha kuhudhuria vikao vya Kamati Kuu ya Chama cha TANU.
 • Alikuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki mwaka 1970 – 1975.
 • Aprili, 1972 aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa kwanza wa Magazeti ya ya Serikali ya Kiingereza ya Daily News na Sunday News.
 • Mwaka 1974 hadi 1976 aliteuliwa kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais.
 • Mwaka 1976 aliteuliwa kuanzisha Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na yeye kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo.
 • Mwaka 1976 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania  nchini Nigeria.
 • Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mbunge wa kuteuliwa.  Aliongoza Wizara hii kwa miaka mitatu  kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa  Habari na Utamaduni, Wizara aliyoiongoza Mwaka 1980 hadi 1982.
 • Mwaka 1982 hadi 1983 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada ambako alifanya kazi kwa muda mfupi kisha mwaka 1983 akahamishwa  na kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani ambako alifanya kazi hadi mwaka 1984.
 • Mwaka 1984 aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, wadhifa alioushika kwa miaka sita (6) hadi mwaka 1990 alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji.
 • Mwaka 1990 hadi mwaka 1992 alikuwa Waziri wa Habari na Utangazaji.
 • Mwaka 1992 alikuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia  na Elimu ya juu wadhifa alioushika hadi mwaka 1995 alipoamua kugombea  na akashinda Urais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi.

FAMILIA

Katika  ndoa yake na Mama Anna, Hayati Benjamin William Mkapa alijaliwa kupata watoto wawili wa kiume Stephan (Steve) na Nicholas (Nico) na wajukuu wawili.

SIASA

 • Hayati Benjamin  William Mkapa  alikuwa Mbuge  wa kuteuliwa mwaka 1977.
 • Mwaka 1985 – 1995 alikuwa Mbunge wa kuchaguliwa wa Jimbo la Nanyumbu Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara.
 • Aidha, kwa miaka mingi alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM; Mjumbe wa Halmashauri Kuu, na Katibu wa Sekretariati ya Mambo ya Nje ya CCM.
 • Novemba, 1995 hadi Novemba, 2005 alichaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika kipindi hicho alikuwa pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.

Hayati Benjamin  William Mkapa alikuwa Rais  wa Kwanza kuchaguliwa chini ya Mfumo wa Vyama Vingi  ulioanzishwa mwaka 1992.

Baadhi  ya Mafanikio ya Hayati Benjamin  William Mkapa Wakati wa Uongozi Wake:

Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Hayati Benjamin William Mkapa pamoja na mambo mengine, alisimamia ipasavyo harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, alijenga mahusiano mazuri ya kimataifa na kusababisha  Tanzania kuungwa mkono na nchi nyingi duniani yakiwemo Mataifa Makubwa kama China na Urussi. Hadi kifo chake Hayati Benjamin William Mkapa aliheshimika sana kwenye nchi za Kusini mwa Afrika kwa kazi kubwa aliyoifanya wakati wa vita vya ukombozi chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, na nyingi ya nchi hizo zilimpa nishani za juu kwa kutambua mchango huo.

Baada ya kuteuliwa kuwa  Rais, Hayati  Benjamin  William  Mkapa alianza kurekebisha uchumi na mifumo ya Serikali  ili kutatua changamoto zilizokuwepo wakati huo.

Katika kupambana  na ufisadi nchini, Hayati Benjamin William Mkapa aliunda TUME ya Rais ya kuchunguza rushwa iliyokuwa chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba mwaka 1996.  Matokeo ya TUME  hii yalisaidia sana kuimarisha vita dhidi ya rushwa nchini na kuanzishwa kwa Taasisi ya kuzuia rushwa nchini.

Hayati Benjamin William Mkapa alichochea marekebisho ya uchumi ikiwemo kuongeza nafasi ya sekta binafsi na ubinafsishaji hasa kwa Mashirika ya Umma ambayo yalikuwa hayajiendeshi vizuri na ambayo yalikuwa yamekufa.   Alianzisha utaratibu aliousimamia mwenyewe wa majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara la Taifa (NBC).

Hayati Benjamin  William Mkapa aliimarisha Sera  za Fedha na kudhibiti mzunguko wa fedha na mfumuko wa bei nchini. Aliongeza sana mapato ya Serikali  na kuimarisha misingi ya uchumi jumla.

Hayati Benjamin William Mkapa alibuni na kuanza kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2000 – 2025 inayotekelezwa hadi sasa. Aidha, alianzisha Taasisi mbalimbali muhimu kuimarisha utendaji wa Serikali zikiwemo:-

 • Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF),
 • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
 • Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
 • Mfuko wa Jamii (TASAF),
 • Tume ya Kupambana na Ugonjwa wa UKIMWI (TACAIDS),
 • Mkakati wa Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA),
 • Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA)
 • Baraza la Biashara la Taifa – National Business Council (NBC) na nyingine nyingi.
 • Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Hayati Benjamin William Mkapa aliimarisha Uhuru wa Vyombo vya Habari na wa kisiasa. Aidha, alitambua na kulenga kuunga mkono mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya Taifa. Ni kwa lengo hilo alikabidhi baadhi ya majengo ya Serikali kwa taasisi hizo ili zianzishe vyuo vikuu kwa mfano alikabidhi majengo ya Shule ya Sekondari Mazengo kwa Kanisa la Anglikana kuanzisha Chuo Kikuu cha St. Johns; alikabidhi majengo ya Chuo cha Benki Iringa kwa Kanisa Katoliki kuanzisha Chuo Kikuu cha Ruaha na majengo ya TANESCO  Morogoro kwa BAKWATA  ili kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislam. Aidha, alikabidhi majengo ya Sekondari ya Magamba kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  Tanzania (KKKT) kuanzisha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa Memorial University (SEKOMU).

Akiwa  Rais, Hayati Benjamin William Mkapa alikuwa:

 • Mwenyekiti  wa Tume ya Dunia ya Kushughulikia Masuala ya Utandawazi.
 • Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Kampuni ya Microsoft Afrika,
 • Mwanzilishi na  mhimili  wa  Kongamano la  Viongozi wa Afrika (African Leadership Forum)  ambalo linajadili changamoto za maendeleo na uongozi Barani Afrika na kutoa ushauri.

KUSTAAFU

Kuanzia  mwaka 2005 baada ya kustaafu,  Hayati Benjamin William Mkapa alikuwa akijishughulisha na masuala mbalimbali kama ifuatavyo;

 • Aliunda Taasisi  yake inayohusika na  kupambana na ugonjwa wa UKIMWI na kuboresha utoaji wa huduma za afya hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi – The Benjamin William Mkapa Foundation (BMF).
 • Mkuu wa Chuo Kikuu cha DODOMA,
 • Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cavendish, Uganda.
 • Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu cha Aga Khan,
 • Mwezeshaji  wa Mazungumzo ya Upatanishi miongoni mwa Vyama  na Makundi ya Kisiasa  yanayohasimiana nchini Burundi,
 • Mjumbe kwenye Kampeni za kuhamasisha kujikinga na UKIMWI kupitia Klabu ya Marais Wastaafu wa Afrika,
 • Mwenyekiti wa Kituo  cha Kusini cha ASASI za Kiserikali  za Nchi zinazoendelea, yaani South Centre,
 • Mjumbe  wa  Kamati  ya Watu Mashuhuri iliyoteuliwa na Katibu  Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na  Maendeleo –  UNCTAD kufanya mapitio ili kuimarisha mchango wa Shirika hilo ndani ya Umoja wa Mataifa,
 • Mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupitia Mfumo wa Utendaji wa Umoja wa Maifa katika maeneo ya Maendeleo, Misaada ya kibinadamu na Mazingira,
 • Mjumbe wa Tume ya Afrika iliyoundwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza (Tony Blair),
 • Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Wanyama Pori Barani Afrika,
 • Kiongozi wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa wakati wa zoezi la kupiga kura za kumaliza mgogoro wa Sudan,
 • Msuluhishi Mwenza na aliyekuwa Rais  wa Nigeria Bw. Olesegun Obasanjo katika mgogoro wa Kisiasa nchini  DRC Kongo, na
 • Msuluhishi Mwenza na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na Mama Graca Machel, Katika Mgogoro wa Kisiasa nchini  Kenya.
 • Mwanzilishi Mwenza wa Investment Climate Facility for Africa.

NISHANI NA TUZO

Hayati Benjamin William Mkapa ametunikiwa  Nishani na TUZO mbalimbali kama ifuatavyo;

 • Mwaka 2005 alitunukiwa TUZO ya Order of the Golden Heart of Kenya (Chief);
 • Mwaka 2007 alitunukiwa TUZO ya Jane Goodall Global Leadership Award;
 • Mwaka 2011 alitunukiwa TUZO ya Order of Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; na nyingine

SHAHADA ZA HESHIMA

Hayati Benjamini  William Mkapa alitunukiwa Shahada mbalimbali za Heshima kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali duniani kama ifuatavyo:-

Hayati Benjamin William Mkapa alikuwa na kauli mbiu zake zilizoakisi fikra zake kuhusu maendeleo ya Taifa na kujitegemea ikiwemo “Ukweli na Uwazi”, “Mtaji wa Maskini ni Nguvu zake Mwenyewe” na kumtegemea Mungu katika kazi kama yeye mwenyewe alivyopenda  kusema “Ora et labora” yaani “Sala na Kazi”. Tumuenzi kwa kuendelea kuongozwa nazo.

UGONJWA NA KUFARIKI

Hayati Benjamin William Mkapa alifariki kwa ugonjwa wa moyo kusimama ghafla (cardiac arrest) tarehe 23 Julai, 2020 majira ya saa 03:30 usiku, akiwa na umri wa miaka 81.

Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa

Jina la Bwana lihimidiwe.

Mkapa Foundation