DAR ES SALAAM, 12 Oktoba 2026 — Katika kufanikisha mchakato wa mabadiliko ya uongozi na uendelevu wa Taasisi, kufuatia maandalizi ya kustaafu kwa Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF), Bodi ya Wadhamini ya Mkapa Foundation imetangaza mpango wa mpito kuanzia Oktoba 2026 hadi Agosti 2027.
Dkt. Mkondya-Senkoro ameongoza Taasisi ya Mkapa Foundation kwa mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006. Katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi wake, BMF imepanua uwigo, na kuongeza ukubwa wa shughuli zake na imegusa maisha ya Watanzania milioni 33 Bara na Zanzibar. Katika kipindi chake; Taasisi imekusanya fedha na kuendesha programu za afya zenye thamani ya takriban shilingi za kitanzania bilioni 500, ikilinganishwa na shilingi milioni 500 ilipoanzishwa mwaka 2006. Aidha, BMF imeweza kubuni miradi iliyotoa ajira kwa watumishi wa afya 19,000 waliosambazwa katika maeneo yenye upungufu wa watumishi wa afya; kutoa ufadhili wa masomo kwa watumishi wa afya 1,200; na kujenga miundombinu ya afya 520, zikiwemo nyumba 480 za watumishi wa afya kwenye maeneo ya pembezoni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMF, Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, amesema “ Nampongeza Dkt. Senkoro kwa kazi mahiri aliyofanya ya kuifikisha BMF ilipo leo.Akiwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kwanza wa taasisi, ametoa mchango mkubwa katika kuijenga taasisi, kujenga madaraja ya ushirikiano na wafadhili na wadau muhimu, na kuifanya taasisi ya kuaminika, inayotumainiwa, na yenye ushawishi mkubwa katika ujenzi wa mifumo ya sekta ya afya kitaifa. Vile vile, Dkt. Ellen aliongoza mikakati ya uendelevu ya taasisi, ikiwemo uanzishaji wa mfuko wa fedha wa kusaidia miradi ya maendeleo na kuendesha taasisi (Endowment Fund) na kampuni tanzu ya “Imara Horizon” na kwa pamoja kusimamia ujenzi wa Jengo la Mkapa Health Plaza katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam. Balozi Mulamula aliendelea kusema: "Mabadiliko haya tunayoyasimamia yanaashiria utayari wetu wa kuyalinda mafanikio makubwa tuliyoyapata na kuhakikisha mustakabali mwema wa taasisi kwa siku za usoni."
Naye Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro alieleza: “Imekuwa heshima kubwa kwangu kuaminiwa na kupewa dhamana ya kushirikiana na watendaji wenzangu, Bodi ya Wadhamini, wafadhili na wadau wote wa maendeleo katika kutimiza malengo ya taasisi hii. Nina imani kubwa juu ya uimara wa taasisi ya BMF na uongozi madhubuti wa Bodi katika kusimamia kipindi cha mpito kuelekea uongozi mpya ifikapo Agosti 2027. Nitatumia kipindi kilichobaki kuiandaa taasisi kwa makabidhiano kwa uongozi ujao”.
Mabadiliko haya ni matokeo ya mpango thabiti na wa muda mrefu ulioanza ndani ya Taasisi mnamo Februari 2026 ili kuimarisha ukuaji na utulivu endelevu. Mchakato huu wa uongozi wa juu unasimamiwa na Bodi kwa kushirikiana na wataalamu wa nje ya Taasisi na tunahahakikisha ushirikishwaji wa wadau muhimu, kuendesha mchakato wa wazi na wa ushindani, na hatimaye makabidhiano tulivu ya kitaasisi. Aidha tangazo la kujaza nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi litatangazwa hivi karibuni.
Bodi inapenda kuwahakikishia washirika, wafadhili, na Umma kwamba, mchakato wa mabadiliko ya uongozi unaendelea pasipo kuathiri dira, tunu, malengo ya Taasisi ya BMF, Mwelekeo wa Kimkakati na utekelezaji wa Programu zote za Taasisi. Aidha tunapenda kuwashukuru kwa ushirikiano wenu katika kuimarisha sekta ya afya na tunaahidi kuendelea kushirikiana nanyi.
Imetolewa na:
Balozi Liberata Mulamula, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini | Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation.
Mawasiliano ya Vyombo vya Habari:
Kitengo cha Mawasiliano, Taasisi ya Benjamin William Mkapa
Barua pepe: info@mkapafoundation.or.tz | Tovuti: www.mkapafoundation.or.tz
LinkedIn: Benjamin William Mkapa Foundation | Instagram: @mkapafoundation | X: @MkapaFoundation
Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMF):
BMF ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa Aprili 2006 na Hayati Benjamin W. Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ni Msarifu. Kuanzia mwaka 2021 nafasi ya Msarifu wa Taasisi hii, ipo chini ya Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,. Malengo makuu ya Taasisi ni kuchangia jitihada za Serikali na Wadau katika kuimarisha mifumo ya afya ili kutoa huduma bora kwa jamii hususan zilizo na uhitaji mkubwa nchini Tanzania na Kanda za Afrika.
Kupata Maelezo zaidi, tazama makala ya Miaka 20 ya BMF inayoangazia miongo miwili ya matokeo chanya chini ya uongozi wa Dkt. Ellen Mkondya Senkoro. https://ig.me/reel/Da5z4sViom7/